logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Profesa Wajackoyah azungumza baada ya kuzuiwa kuwania urais

Wajackoyah alikuwa na orodha kamili ya wafuasi kutoka kaunti 17 kati ya 24 zinazohitajika.

image
na Radio Jambo

Habari30 May 2022 - 19:56

Muhtasari


•Wakili huyo ambaye ana umri wa miaka 61 alikuwa na orodha kamili ya wafuasi kutoka kaunti 17 kati ya 24 zinazohitajika.

•Wajackoyah amewahakikishia wafuasi wake kuwa watawasilisha stakabadhi zilizokosekana haraka iwezekanavyo.

Mgombea urais George Wajackoyah katika BOMAS ya Kenya Jumatatu, Mei 30, 2022.

Siku ya Jumatatu mgombea urais kwa tikiti ya Roots Party George Wajackoyah alikataliwa na tume ya IEBC kwa kukosa kuwasilisha idadi inayohitajika ya saini za wafuasi.

Wakili huyo ambaye ana umri wa miaka 61 alikuwa na orodha kamili ya wafuasi kutoka kaunti 17 kati ya 24 zinazohitajika.

Wajackoyah alikuwa miongoni mwa wagombea urais waliotazamiwa kukutana na Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati Jumatatu katika ukumbi wa Bomas of Kenya.

IEBC ilimpatia mhadhiri huyo wa chuo kikuu hadi Alhamisi kuwasilisha orodha zote kamili zinazohitajika ili kuruhusiwa kuwania urais.

Akizungumza baada ya mkutano wake na tume ya uchaguzi,Wajackoyah aliwahakikishia wafuasi wake kuwa watawasilisha stakabadhi zilizokosekana haraka iwezekanavyo.

Kiongozi huyo wa Roots Party ambaye ambaye alikuwa ameandamana na mgombea mwenza wake Justina Wambui Wamae pia alibainisha kuwa walikuwa wamekidhi mahitaji mengine yote yaliyoorodheshwa na IEBC.

"Tutakuja haraka iwezekanavyo. Hata hivyo tunawahakikishia wafuasi wetu kuwa ukipata kila kitu ni safi, basi kuna shida mahali. Angalau kuna kosa ambalo limefanyika ama kuna upungufu fulani, tutafanya hilo. Tumepita kila kitu kingine, hako kengine kadogo tutafanya hivyo," Wajackoyah alisema.

Wambui aliongeza kuwa tayari wako na data zinazohitajika na akawahakikishia kuwa watakuwa wameziwasilisha kwa tume kabla ya Juni 2.

Wajackoyah alizaliwa katika eneo la Magharibi mwa Kenya na anazamia kuwa rais wa tano baada ya rais Kenyatta kustaafu mwezi Agosti.

Ahadi yake  ya kuhalalisha Bangi iwapo atashinda uchaguzi wa Agosti 9 imezua hisia tofauti kwenye mitandao ya kijamii lakini amedhamiria kutimiza lengo lake.

Hii si mara ya kwanza kwa Wajackoyah kumezea mate kiti cha urais.

Mwaka wa 2013 alitangaza kwamba angegombea Urais, lakini alijiondoa dakika za mwisho bila maelezo yoyote.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved