Naibu rais William Ruto ajiondoa kwenye mjadala wa urais

Muhtasari

• "Chini ya mazingira ya sasa ya vyombo vya habari vinavyoegemea upande mmoja, tumemshauri mgombea wetu kutoshiriki katika mdahalo wa urais."

Image: FACEBOOK// WILLIAM RUTO

Chama cha UDA kimemshauri Naibu Rais William Ruto kujiondoa kwenye mjadala wa urais utakaoandaliwa mwezi Julai. 

Katika taarifa yake siku ya Alhamisi, Mkuu wa Mawasiliano wa UDA Hussein Mohammed alisema hii ni kutokana na mapendeleo ya vyombo vya habari. 

"Tumeona kwa wasiwasi mwingi mapendeleo yanayorudiwa na yanayoendelea pamoja na propaganda katika baadhi ya vyombo vya habari vya Kenya katika matumizi mabaya ya sheria," alisema. 

"Chini ya mazingira ya sasa ya vyombo vya habari vinavyoegemea upande mmoja, tumemshauri mgombea wetu kutoshiriki katika mdahalo wa urais."

Mjadala wa urais hauandaliwi na kituo chochote cha habari. Muungano wa wamiliki wa Vyombo vya Habari, Baraza la Habari la Kenya na Chama cha Wahariri wa Kenya kwa pamoja walitangaza kwamba mijadala ya Rais na Naibu Rais itafanyika kabla ya uchaguzi. Taasisi hizo zilisema tarehe maalum, ukumbi na vifaa vitatangazwa baadaye. 

"Inapangwa kufanyika Julai kwa mashauriano na vyama vya kisiasa kabla ya Agosti 9, 2022. Pia kundi la wahariri wakuu kutoka vyombo mbalimbali vya habari limeundwa ili kuzingatia maslahi ya Wakenya na kutoa haki kwa wote wanaohusika. " walisema katika taarifa ya pamoja. 

Wakati wa mdahalo huo, hadhira ya moja kwa moja inayowakilisha sekta mbalimbali za jamii itakuwepo na wananchi watakuwa na jukwaa la kutuma maswali yao pia. 

Ni katika jukwaa hilo ambapo wagombea hao wanatarajiwa kuuza ajenda zao na kile ambacho wamewekea Wakenya kabla ya uchaguzi mkuu ujao.