Wapiga kura 800,000 wameondolewa kwenye sajili ya IEBC katika njama ya wizi wa kura- Ruto

Muhtasari

•Ruto alisema takriban majina 800,000 yametoweka kwa njia isiyoeleweka kutoka kwa sajili hiyo ambayo iko hadharani.

•Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amepuuzilia mbali madai ya Ruto akisema hakuna data iliyopotea kutoka kwa sajili ya wapiga kura.

Naibu rais William Ruto
Naibu rais William Ruto
Image: EZEKIEL AMINGA

Naibu Rais William Ruto amedai kuwa takriban wapiga kura milioni moja waliosajiliwa katika ngome zake wameondolewa kwenye sajili ya IEBC.

Akizungumza alipokutana na mabalozi wa EU siku ya Alhamisi, Ruto alisema takriban majina 800,000 yametoweka kwa njia isiyoeleweka kutoka kwa sajili hiyo ambayo iko hadharani.

“Tutachukua msimamo kuhusu suala hili. Tunaandikia IEBC kwa sababu kulikuwa na jaribio la kufuta majina kutoka kwa sajili ya IEBC,” alisema.

"Ni hatari, haswa wakati maafisa wa umma wanapopiga kifua kwamba serikali kuu itasimamia uchaguzi."

Lakini mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amepuuzilia mbali madai ya Ruto akisema hakuna data iliyopotea kutoka kwa sajili ya wapiga kura.

Ruto alisema yuko tayari kufanya kazi na IEBC kuhakikisha kuwa Kenya itatekeleza uchaguzi wa kuaminika.

"Tunatarajia kwamba EU itajaribu kupata maelezo mengi kutoka kwa IEBC na maafisa wa umma kuhusu jinsi majina milioni moja yalitoweka," alisema.

“Majina mengi ni ya watu kutoka ngome zetu. Kuna jaribio la wazi la kujaribu baadhi ya michezo ya tumbili. Hawatafaulu lakini majaribio haya yanatia wasiwasi Wakenya.”

DP pia aliisihi EU kuangalia "njia za ajabu ambazo baadhi ya watu wanataka kuzitumia kuiba uchaguzi" mwezi Agosti.

“Kuna watendaji serikalini wanaotaka kuhujumu uwezo wa IEBC. Wanataka kwenda kinyume na uchaguzi huru na wa haki na hilo halikubaliki nchini Kenya,” alisema.

Ruto alisema maafisa wa umma hawafai kuegemea upande wowote wa kisiasa, kinyume na kiapo chao cha kuhudumu.

"... Sio tu kwamba wanahujumu katiba lakini ni maajenti mahiri wa kuhujumu uchaguzi wa uwazi," alisema.

Ruto alidai kuwa maafisa wa Umma wanaosimamia ICT katika IEBC pia wanadai kuwa wana data zinazoweza kubaini nani anashinda au ni nani atashindwa katika uchaguzi.

"Wanasema wanasimamia data ambayo itafanya upande wowote kushinda. Hiyo inadhoofisha uchaguzi wa kuaminika. Tunatarajia marafiki wa Kenya, EU kuzungumza na masuala ya uchaguzi wa kuaminika,” alisema