Serikali yangu haitakopa mikopo kwa ajili ya miradi-Ruto asema

Muhtasari
  • Mgombea urais wa Kenya Kwanza William Ruto sasa anasema kukopa pesa za kuendesha serikali haitakuwa chaguo kwa serikali yake
Image: DP RUTO/TWITTER

Mgombea urais wa Kenya Kwanza William Ruto sasa anasema kukopa pesa za kuendesha serikali haitakuwa chaguo kwa serikali yake.

Ruto alifichua kuwa wakati muungano wa Azimio unaoongozwa na Raila Odinga unapanga kuendelea na ukopaji mkubwa wa mikopo, chao ni kutumia chaguzi za ndani ili kupata mapato.

"Tutabadilisha utamaduni huu wa kutuma maombi ya mikopo na tujishughulishe na uwekezaji na programu zinazohitaji wafanyakazi wengi tofauti na miradi inayohitaji mtaji," alisema Ijumaa alipokuwa kwenye mkutano wa kampeni Kamulu, Nairobi.

Ruto alisema mpango wa ujenzi wa nyumba nchini utasaidia wale wote ambao watajenga nyumba Nairobi na Kenya kote kwa jumla.

"Hii ni ili tuweze kuhakikisha kuwa Wakenya wengi wanajenga nyumba na kuongeza umiliki wa mali nchini Kenya na raia wengi wa nchi yetu kuu," alisema.

Ruto ambaye alikuwa kwenye kampeni jijini Nairobi alisema atasaidia wafanyikazi wa jua kali kupata uzalishaji wa juu zaidi.

"Tutasaidiana na wale wanajenga manyumba Nairobi. Badala ya wewe mwananchi kulipa rent ya elf nane kila siku utalipa mortgage ya elfu nane baada ya miaka kumi ama kumi na tano nyumba inakuwa yako. Hakuna haja ya wewe kupanga nyumba miaka yote," Alisema.

"Tutabadilisha jina na kuwa viwanda kwa sababu huko ndiko tunakofanya uzalishaji mkubwa. Tutatumia sekta ya jua kali kuleta mapinduzi ya viwanda nchini mwetu, " alisema.

Ruto pia aliahidi kujenga vibanda vya wafanyikazi wa jua kali wanaofanya kazi katika maduka ya muda kando ya barabara ili kuwasaidia kupata uzalishaji wa juu zaidi.

"Tunataka kuongeza thamani, usindikaji wa mazao ya kilimo na kuongeza utajiri wetu. Tutaondoa umaskini na kujenga Kenya ambayo sote tunajivunia," Ruto alisema.

Alisema hii ni kuhakikisha kuwa Mkenya wa kawaida anajilimbikizia mali.Alisema pia itasaidia kutatua suala la ukosefu wa ajira ambalo linawakabili vijana.

DP ameahidi kuwa serikali yake itatenga Sh100 bilioni mfuko ambao utasaidia mamilioni ya vijana kwa kuwapa mitaji ya kuanzisha biashara na kujitengenezea ajira.