Irungu Kang'ata anyimwa kibali cha kuwania ugavana wa Murang'a

Muhtasari

•Hii ni baada ya tume hiyo kubaini kuwa mgombea mwenza Winnie Mwangi alikosa kujiuzulu ndani ya muda uliowekwa kisheria.

•EACC ilituma barua kwa IEBC ikionyesha kuwa Mwangi hakujiuzulu kabla ya Februari 9 kama inavyotakiwa kisheria.

Seneta Irungu Kang'ata
Image: MAKTABA

Tume huru  ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC)  imemnyima Seneta wa Murang’a  Irungu Kang'ata  kibali cha  kuwania kiti cha ugavana wa Murang'a.

Hii ni baada ya tume hiyo kubaini kuwa mgombea mwenza Winnie Mwangi alikosa kujiuzulu ndani ya muda uliowekwa kisheria.

Katiba iliwataka maafisa wa serikali wanaotafuta viti vya kuchaguliwa katika uchaguzi wa Agosti 9 kujiuzulu kabla ya Februari 9, 2022.

Mwangi alikuwa akifanya kazi  ya uhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi kwa zaidi ya miaka 25 kabla ya kuchaguliwa kuwa mgombea mwenza wa Kang'ata.

EACC ilituma barua kwa IEBC ikionyesha kuwa Mwangi hakujiuzulu kabla ya Februari 9 kama inavyotakiwa kisheria.

Lakini Kang'ata alitaja hatua hiyo kuwa uchochezi na kuwalaumu wapinzani wake ambao alisema wameungana katika jaribio la kumzuia kuwania kiti cha ugavana.

"Tuna ushahidi kwamba alijiuzulu kwa wakati na tutarejea kesho kuthibitisha," alisema.

Kang'ata anawania kiti hicho dhidi ya wagombea wengine watano kupitia tikiti ya chama cha UDA.

(Utafsiri: Samuel Maina)