Wagombea waliofungiwa nje ya kinyang’anyiro cha urais wasema ‘Hawatanyamazishwa’

Muhtasari
  • Wagombea waliofungiwa nje ya kinyang’anyiro cha urais wasema ‘Hawatanyamazishwa’
Image: WILFRED NYANGARESI

Baadhi ya wawaniaji urais ambao hawakushiriki katika kinyang'anyiro cha Agosti hadi Ikulu wamelia kwa kile wanachodai ubaguzi wa IEBC dhidi ya wagombeaji kwa "sauti mbadala".

Wakiongozwa na Jimi Wanjigi wa Chama cha Safina ambaye uteuzi wake ulitupiliwa mbali Jumatatu na baraza la uchaguzi kwa kukosa shahada ya chuo kikuu, wagombeaji hao wanadai kuwa tume hiyo ina nia ya "kuwanyamazisha".

"Tumeona kiolezo hiki hapo awali na ni kiolezo cha udikteta. Ninataka kuwahakikishia Wakenya kwamba ilishindwa hapo awali na tutaishinda tena sasa,” amesema Bw Wanjigi kwenye kikao na wanahabari Jumanne.

Alishutumu serikali kwa "kuwanyamazisha" raia wanaojitokeza kubadilisha hali ilivyo, kupitia mashirika ya Serikali kama vile IEBC.

Wakati uo huo, mwimbaji wa nyimbo za injili Reuben Kigame aliikashifu tume hiyo kwa madai ya kuwabagua watu wanaoishi na ulemavu.

“Chebukati na timu wamenibagua. Jambo baya zaidi la ubaguzi huo ni kwamba ametangaza wagombeaji 4 kwenye gazeti la serikali na kutoa orodha ya wagombeaji ambao hawakuhitimu. Wakenya, mnajua kwamba sionekani katika orodha zote mbili?” Kigame ambaye ni mlemavu wa macho aliwauliza waandishi wa habari.

“Hilo linakuambia nini? Huyo chebukati na timu wananichukulia kama chombo, kama ajali. Wanawatendea watu wenye ulemavu kwa dharau. Haitatokea kwa sababu hatutanyamazishwa.”

Kwa upande wake, mpeperushaji bendera wa Thirdway Alliance Ekuru Aukot, ambaye anawania urais kwa mara ya tatu alisema bodi inayoongozwa na Wafula Chebukati ilikuwa na nia ya kutatiza azma yake ya urais mwaka huu, baada ya kumuondoa hapo awali.

“Mwaka wa 2017 IEBC ilinipa cheti cha kuwania urais. Jumapili iliyopita, IEBC ilininyima cheti hicho kwa kisingizio kwamba cheti changu cha digrii hakijaidhinishwa, si jambo la kuchekesha?” Dk Aukot amesema.

"Nadhani tunashughulika na taasisi hapa ambayo inafuta wagombea wasiofaa kwa sababu tu hawataki sauti mbadala."

Aidha aliapa kuwashtaki makamishna wote wa IEBC akisema: “Binafsi, nitawasilisha kesi dhidi ya kila mmoja wa makamishna hao kwa sababu watu hawawezi kufanya maamuzi ambayo yanadhuru watu na kujificha nyuma ya taasisi inayoitwa IEBC.”