Wanapewa pesa kidogo-Wajackoyah awataka viongozi kuacha kuwatumia vijana kusababisha fujo

Muhtasari
  • Wajackoyah awataka viongozi kuacha kuwatumia vijana kusababisha fujo
Image: CHARLENE MALWA

Kiongozi wa Roots Party Prof George Wajackoyah amewasuta washindani wake akisema wanakuza tabia mbovu kwa vijana.

Akizungumza katika mahojiano na Radio Jambo siku ya Ijumaa, Wajackoyah alishutumu viongozi hao kwa kutumia vijana wengi waliohitimu masomo yao wasio na ajira kusababisha fujo.

"Wanapewa tu pesa kidogo waende warushie watu mawe. Na ukiona siasa za leo, wale tunapingana nao kazi yako ni kutusiana," Wajackoyah alisema.

Wajackoyah alisema vijana wanaopania kujitosa katika siasa wataishia kufuata nyayo na mifano iliyokuwa ikitolewa na watangulizi wao.

Aliongeza kuwa suluhisho lake la ukosefu wa ajira ni la kweli zaidi kuliko lile linalotolewa na wagombea wengine wa urais.

Aliwaambia wananchi wajitolee katika kuchuma toroli za Naibu Rais William Ruto, ili wazitumie kusafirisha miche ya bangi mnamo Agosti 9.

"Wamekuwa wakiwaambia watu watatengeneza ajira kwa miaka 50 iliyopita katika kila msimu wa kisiasa. Watapata wapi ajira hizo?" Aliuliza.