Aliyekuwa seneta wa Kakamega Boni Khalwale alikumbana na ghadhabu ya wakazi katika eneo la Matungu, kaunti ya Kakamega.
Tukio la mtafaruku lilizuka na kupelekea gari lake kutupiwa mawe alipokuwa akikimbia kwa kasi kuokoa maisha yake.
Masabu yalianza baada yake kukosa kumuidhinisha Seneta Cleophas Malala kuwania kiti cha ugavana licha ya wote wawili kuwa katika Muungano wa Kenya Kwanza.
Seneta huyo wa Zamani aliwataka wakazi kuwapima viongozi wote kutoka eneo hilo na kumchagua yeyote wanayemtaka kwa wadhifa wowote.
Hata hivyo, alijipigia debe huku akijigamba kuwa yeye ndiye mtunzi sheria bora anayejulikana kote nchini.
"Sote tunatafuta viti. Tupimeni na mmchague yeyote ambaye mnamtaka kwa kiti chochote. Chagua atakayekujali. Kumbuka Khalwale ndiye mtunzi sheria bora nchini Kenya."
Matamshi hayo yalimzonga Malala ambaye alikabiliana naye uso kwa uso akisema "amechanganyikiwa".
Ni baada ya makabiliano hayo ambapo Khalwale alilazimishwa kutoroka mkutano huo na wafuasi wa Malala waliokuwa wamejawa na hasira.
"Ondoka hapa. Toweka," seneta huyo aliamrishwa na vijana wenye ghasia kwenye video iliyofikia Radio Jambo.
Huku walinzi wake wa usalama wakisafisha njia, kundi lililokuwa na ghadhabu lilifuata gari lake likimwambia aharakishe.
Mambo yalizidi kuwa mabaya baada ya kundi hilo kuanza kurusha mawe kuelekeza kwenye msafara wake.
Hatimaye seneta huyo alifanikiwa kuondoka katika eneo hilo la ghassia huku vijana hao wakiendelea kurushia mawe gari lake.
Baada yake kuondoka eneo la tukio, vijana hao walisikika wakiimba: "Tunamtaka Lishenga! Tunataka lishenga!"
Lishenga ndiye mgombeaji wa ODM kwa kiti cha useneta wa Kakamega.