logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Hutabadili nia ya wakazi wa Nairobi!- Sakaja amkashifu DCI Kinoti

Kinoti alisema kuwa wanapanga  kuwasilisha kesi dhidi ya Sakaja.

image
na

Burudani17 June 2022 - 07:33

Muhtasari


•Sakaja alisisitiza kuwa hakuna  vitisho vya aina yoyote ambavyo vitabadilisha nia ya  wakazi wa Nairobi ya kupata uongozi mpya

•Kinoti alisema kuwa wanapanga  kuwasilisha kesi dhidi ya Sakaja Iwapo atapatikana na hatia ya kughushi karatasi zake za chuo kikuu.

Johnson Sakaja

Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja  amesema kwamba hatakubali vitisho vya kukamatwa kutoka kwa  DCI George Kinoti.

Katika taarifa aliyotoa Ijumaa, Sakaja alisisitiza kuwa hakuna  vitisho vya aina yoyote ambavyo vitabadilisha nia ya  wakazi wa Nairobi ya kupata uongozi mpya.

“Vitisho vya kukamatwa na kuteswa na serikali havitatutisha wala kubadili nia ya wakazi wa Nairobi. Azimio letu linasalia thabiti, " Sakaja alisema kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Sakaja alisisitiza  kuwa  vyeti vyake vya Elimu ni halali huku akidai kuwa taasisi husika zimekataa kuitikia wito wa bosi wa DCI.

“Bwana DCI Kinoti, niko katika afisi yangu ya Riverside, karibu au nijulishe ikiwa ungependa nije. Afisi yako haitalazimisha  mtu  kwa wakazi wa Nairobi,”  Sakaja alisema.

Sakaja alikuwa akimjibu Kinoti ambaye Alhamisi alisema kuwa wanachunguza iwapo Sakaja ni mmoja wahalifu wa kimataifa kufuatia utata uliozingira cheti chake cha shahada.

Akiongea na Daily Nation, Kinoti alisema kuwa wanapanga  kuwasilisha kesi dhidi ya Seneta huyo Iwapo atapatikana na hatia ya kughushi karatasi zake za chuo kikuu.

"Hatutasalimisha mji wetu mkuu kwa wadanganyifu. Tutahusisha mashirika yote ya kimataifa katika kuchunguza na kumfungulia mashtaka yeyote aliyehusika katika udanganyifu wa kitaaluma," Kinoti alisema.

Azma ya Sakaja kuwania  Ugavana wa Nairobi Imekwama baada ya malalamishi manne kuwasilishwa mbele ya Kamati ya Kutatua Mizozo ya IEBC kupinga stakabadhi zake za masomo alizowasilisha kwa tume hiyo ili kuidhinishwa kuwania Ugavana.

Wakati wa kesi hiyo, mawakili wake walitaka itupiliwe mbali kwa kuwa walalamishi hawakufika mahakamani.

Malalamiko matatu kati ya manne yaliyowasilishwa dhidi ya seneta huyo wa awamu ya kwanza yalitupiliwa mbali.

Evans Kaita, Alex Abere na Elizabeth Nzisa, walitaka Kamati hiyo kutupilia mbali kibali cha Sakaja kuwania kiti cha ugavana wa Nairobi kwa msingi kwamba hana sifa zinazohitajika za kitaaluma kuwania kiti hicho.

Kamati ya kusuluhisha mzozo  pia ilitupilia mbali barua ya Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu vilivyotambua shahada ya Sakaja.

Mahakama Kuu katika kesi ya uhakiki  pia iliahirisha uamuzi wa CUE kubatilisha kutambuliwa kwa shahada ya Sakaja

Mahakama iliagiza CUE kudumisha uhalali wa shahada ya Sakaja ikisubiri mwelekeo zaidi wa mahakama

Mahakama pia ilizuia IEBC kufutilia mbali jina la Sakaja kwenye orodha ya wawaniaji walioidhinishwa kuwania kiti cha ugavana.

Hata hivyo, mahakama hiyo ilisema Sakaja atajua hatima yake ya kugombea kwake Jumapili saa nane jioni.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved