Msiwachague viongozi wanaomdharau Uhuru, Karua sema

Muhtasari
  • "Hata nilipokuwa chini ya uongozi wa aliyekuwa Rais Mwai Kibaki, sikuwahi kumvunjia heshima. Niliondoka kwa heshima aliyokuwa amenipa," aliongeza.
Image: MARTHA KARUA/TWITTER

Mgombea mwenza wa urais wa Azimio Martha Karua amewaonya Wakenya dhidi ya kuwapigia kura viongozi ambao wamekuwa wakikosa heshima kwa Rais Uhuru Kenyatta.

Akizungumza wakati wa mkutano wa kampeni huko Gatanga siku ya Ijumaa, Karua alisema ni makosa kwa viongozi kumtusi Rais, na kuwataka wakazi waepuke tabia hizo.

Kiongozi wa Narc, katika kile kilichoonekana kama matamshi yaliyoelekezwa kwa kiongozi wa Kenya Kwanza William Ruto, alisema ikiwa mmoja ni naibu, wanapaswa kusalia katika safu ya majukumu yao.

"Mimi sijasema usikosoe. Ata kama ni rais kosoa. Lakini ukosoe kwa heshima na kwa misingi ya sababu za kutosha."

"Hata nilipokuwa chini ya uongozi wa aliyekuwa Rais Mwai Kibaki, sikuwahi kumvunjia heshima. Niliondoka kwa heshima aliyokuwa amenipa," aliongeza.

Karua aliwataka wazazi kutokubali kudharauliwa na pia kuwafundisha watoto wao kuhusu fadhila ya heshima.

"Ni nani kati yenu wazazi angeruhusu watoto wao kuwadharau? Heshima ni fadhila."

Aliongeza kuwa yeye na wenzake katika Muungano wamekuza kuheshimiana wao kwa wao na wao wenyewe, na hilo linapaswa kuigwa katika vyama vingine.