Afueni kwa Sakaja baada ya IEBC kutupilia mbali kesi ya Digrii

Muhtasari

•"Nimefurahi kwamba tumethibitishwa, tumefuzu, tuna sifa zinazohitajika kuwania wadhifa wa ugavana wa Nairobi," Sakaja alisema.

•Kamati hiyo pia ilitupilia mbali ombi lililopinga uhalali wa mgombea kiti cha ugavana wa Machakos Wavinya Ndeti kuhusu sababu sawa.

Mgombea Ugavana wa Naairobi Johnson Sakaja mbele ya Kamati ya IEBC ya Kusuluhisha Mizozo katika Mahakama ya Milimani mnamo Juni 15 2022.
Mgombea Ugavana wa Naairobi Johnson Sakaja mbele ya Kamati ya IEBC ya Kusuluhisha Mizozo katika Mahakama ya Milimani mnamo Juni 15 2022.
Image: DOUGLAS OKIDY

Mgombea ugavana wa Nairobi Johnson Sakaja ameidhinishwa na Kamati ya Kusuluhisha Mizozo ya IEBC kuwania kiti hicho kwenye uchaguzi wa Agosti.

Hii ni baada ya mahakama hiyo kutupilia mbali ombi lililopinga uhalali wa shahada yake.

Mnamo Jumapili kamati hiyo ilisema haina mamlaka ya kubainisha uhalisi wa stakabadhi hiyo.

"Nimefurahi kwamba tumethibitishwa, tumefuzu, tuna sifa zinazohitajika kuwania wadhifa wa ugavana wa Nairobi," Sakaja alisema.

"Tuko ndani ya kushinda ili tuweze kubadilisha jiji letu hili kubwa," aliongeza mara baada ya hukumu hiyo kutolewa.

Mlalamishi, Dennis Wahome, aliwasilisha kesi mbele ya mahakama hiyo akidai kwamba shahada ya Sakaja ya Sayansi katika Usimamizi kutoka Chuo Kikuu cha Team nchini Uganda ilikuwa ya kughushi.

Alitaka cheti cha kibali cha seneta huyo kilichotolewa Julai 7, 2022 na IEBC kubatilishwa kwa msingi kuwa hana sifa ya kuwania kiti cha ugavana.

Sheria ya Uchaguzi inaweka sharti kwa mtu anayewania kiti cha ugavana kuwa mwenye shahada kutoka chuo kikuu kinachotambuliwa nchini Kenya.

Hapo awali, kamati hiyo pia ilitupilia mbali ombi lililopinga uhalali wa mgombea kiti cha ugavana wa Machakos Wavinya Ndeti kuhusu sababu sawa.