Pigo kwa Sonko baada ya IEBC kukataa ombi lake kuruhusiwa kuwania ugavana Mombasa

Muhtasari

•Kamishna wa IEBC Justus Nyang'aya  alisema kuwa mlalamishi alikosa kuwasilisha cheti halisi cha digrii ili aidhinishwe.

•Sonko hata hivyo, atasubiri uamuzi wa mahakama ya Juu ili kujua hatima yake.

Gavana wa zamani wa Nairobi Mike Sonko
MIKE SONKO Gavana wa zamani wa Nairobi Mike Sonko
Image: BRIAN OTIENO

Kamati ya IEBC ya Kusuluhisha Mizozo imekubali uamuzi wa afisa wa uchaguzi wa Mombasa wa kumzuia Mike Sonko kuwania ugavana.

Jopo katika uamuzi wake lilisema mlalamishi alishindwa kutoa sababu za msingi za "kuvuruga uamuzi wa msimamizi wa uchaguzi" wa kukataa ombi lake.

"Malalamiko hayana uhalali na kwa hivyo yametupiliwa mbali," Wambua Kilonzo alisema wakati akitoa uamuzi Jumatatu.

Kamishna wa IEBC Justus Nyang'aya ambaye alisoma uamuzi wa jopo hilo alisema kuwa mlalamishi alikosa kuwasilisha cheti halisi cha digrii ili aidhinishwe.

Nyang'aya alisema kama ilivyoainishwa katika Kifungu cha 22 (1) (b) ni lazima mtu awasilishe cheti cha shahada ambacho ni sharti linalowabana waombaji wote na anayetaka kuwasilisha alikuwa chini ya wajibu wa kuwasilisha.

“Cheti ambacho kinakubaliwa na IEBC kwa madhumuni ya uchaguzi mkuu wa 2022 ni uthibitisho wa taasisi inayotoa stakabadhi hiyo,” alisema.

Alibanisha kuwa uidhinishwa na wakili hairuhusiwi ingawa alitumia hati hiyo hiyo kwa kibali katika uchaguzi wa 2017.

"Hakuna chochote kilichowekwa mbele ya tume hii kuthibitisha kuwa mlalamishi ana cheti cha digrii," Nyang'aya alisema.

Hata hivyo, alisema mlalamikaji aliwasilisha cheti chake baadaye siku ya mwisho ya zoezi hilo, ilifanyika mwendo wa saa kumi unusu jioni ambapo ilikuwa nje ya muda uliopangwa.

"Mlalamishi alitoa cheti cha shahada lakini alishindwa kuwasilisha saa kumi alasiriili kuzingatiwa," alisema.

Alisema kuhusu suala la kung’atuliwa mamlakani ni lazima liungwe mkono na amri kutoka kwa mahakama.

Sonko, kwenye malalamishi yake, alidai kuwa haikuwa sawa kwa msimamizi wa uchaguzi kumkataza licha ya rufaa yake iliyowasilishwa katika Mahakama ya Juu dhidi yake kuhusu kung’atuliwa kwake.

Katika kuunga mkono hoja yake kwamba aliwasilisha barua hiyo kutoka kwa mahakama, Sonko hata alitayarisha kanda tatu za video za jopo hilo.

Moses Kipkogei ambaye alikuwa amejitokeza katika IEBC aliwasilisha kwamba mwaniaji huyo kushindwa kuwasilisha cheti chake cha digrii, nakala iliyoidhinishwa ya cheti hicho kutoka kwa taasisi husika na ukiukaji wa Kipengee cha 75 cha Katiba ndio sababu za kukataliwa kwa wadhifa wake.

Wilfred Nyamu ambaye alimwakilisha Sonko pamoja na Dan Maanzo, na Kevin Katisya miongoni mwa wengine walikuwa wamesema hakuna sharti kisheria kwamba nakala iliyoidhinishwa ya cheti hicho lazima iwasilishwe.

“Mgombea hajapewa nafasi ya kujitetea...mwenyekiti wa IEBC amepuuza haki zote za kimsingi za mwananchi, alitunga sheria kiholela na kuhatarisha chama cha Wiper,” Katisya aliambia kamati wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Katisya alisema msimamizi wa uchaguzi alitenda isivyo haki kwa kutumia viwango viwili.

Hatua ya mwisho ya IEBC sasa inaweka hatma ya Sonko katika sintofahamu.

Sonko, hata hivyo, atasubiri uamuzi wa mahakama ya Juu ili kujua hatima yake.

Anatafuta maagizo ya kufutilia mbali uamuzi wa tume hiyo wa kutomuondoa kuwania kiti cha ugavana Mombasa