Uhuru kuongoza mkutano wa baraza kuu la muungano wa Azimio

Muhtasari

• Rais Kenyatta ambaye ni Mwenyekiti wa baraza hilo, alisema kuwa mkutano huo utaongozwa na kiongozi wa chama na mgombea urais Raila Odinga.

RAIS UHURU KENYATTA
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta ameitisha mkutano wa baraza kuu la muungano wa Azimio la Umoja One Kenya leo Ijumaa.

Mkutano huo ambao ni wa pili wa aina yake kuitishwa na Rais Kenyatta baada ya ule wa kwanza kufanywa Aprili 21 kwa muda wa wiki moja kufuatia usajili rasmi wa chama cha muungano, utaandaliwa juma la KICC nyakati za alasiri.

Rais Kenyatta ambaye ni Mwenyekiti wa baraza hilo, alisema kuwa mkutano huo utaongozwa na kiongozi wa chama na mgombea urais Raila Odinga.

Miongoni mwa ajenda za mkutano huo, ni pamoja na kudurusu, kutunga na/au kuidhinisha sera za chama.

Baraza la muungano pia limepangwa kupitia mkakati na mpango wa kampeni za chama, ili kuhakikisha Odinga anashinda kinyang'anyiro cha urais 2022, na vile vile kuhakikisha Azimio anaunda serikali ijayo na wingi wa Bunge katika mabunge yote 47 ya kaunti.

Miongoni mwa wajumbe wa baraza la muungano wanaotarajiwa kuhudhuria ni pamoja na: mgombea mwenza wa Odinga na kinara wa Narc-Kenya Martha Karua, Kalonzo Musyoka wa Wiper, Mwenyekiti wa KANU Gideon Moi, Gavana wa Kitui Charity Ngilu na mwenzake wa Mombasa Hassan Joho.

Wengine ni Mbunge wa Taveta Naomi Shaban, mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi, Mwakilishi wa Wanawake wa Murang’a Sabina Chege, Abdi Noor Omar Farah na Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed, ambaye ni Katibu Mkuu wa Halmashauri Kuu ya Muungano wa Kitaifa wa chama hicho.