CJ Martha Koome anaunda benchi la majaji 3 kusikiliza ombi la Sonko dhidi ya chama cha Wiper

Anatafuta maagizo ya kuzuia tume hiyo kutochapisha karatasi za kupigia kura

Muhtasari

•Anatafuta maagizo ya kuzuia tume hiyo kutochapisha karatasi za kupigia kura za wadhifa wa ugavana wa Mombasa katika uchaguzi mkuu ujao wa Agosti 9.

•Jaji Mkuu Martha Koome ameunda benchi ya majaji watatu kusikiliza na kuamua ombi la aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko.


Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko
Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko
Image: Facebook// Mike Sonko

Jaji Mkuu Martha Koome ameunda benchi ya majaji watatu kusikiliza na kuamua ombi la aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko.

Chifu huyo wa zamani wa kaunti anatafuta maagizo ya kuzuiwa chama cha Wiper Democratic kumteua mgombeaji  mwingine  kuchukua  nafasi yake katika kinyang'anyiro cha ugavana Mombasa.

Katika barua iliyoandikwa Juni 29 iliyotiwa saini kwa niaba yake na afisi ya mawakili mkuu wa jaji mkuu, Koome alidhibitisha  kuwa ameteuwa majaji watatu kusikiliza na kuamua suala hilo mjini Mombasa.

"Asante kwa barua yako ya Juni 27 mwaka huu iliyotumwa kwa mheshimiwa Jaji Mkuu. Nina maagizo ya kukujulisha kwamba CJ amepokea faili ya awali ya mahakama kutoka mahakama kuu ya Mombasa", sehemu ya barua hiyo ilidokeza.

Mnamo Ijumaa wiki jana, jaji wa Mahakama Kuu ya Mombasa Olga Sewe katika uamuzi wake, aliamuru kesi hiyo ipelekwe mbele ya Jaji Mkuu ili kumwezesha kuunda benchi ya kusikiza na kuamua kesi hiyo kwani inazua maswali makubwa ya sheria.

Katika kesi hiyo iliyowasilishwa katika mahakama kuu ya Mombasa, Sonko alidai kuwa  huenda akapata hasara kubwa ikizingatiwa kiasi cha pesa na muda aliowekeza katika azma yake ya kuwania kiti cha Ugavana.

Hasara hiyo anadai itatokana na kuisha kwa saa 72 zilizoruhusiwa na IEBC kwa chama hicho kusimamisha mgombeaji mpya kwa nafasi yake.

Anatafuta maagizo ya kuzuia tume hiyo kutochapisha karatasi za kupigia kura za wadhifa wa ugavana wa Mombasa katika uchaguzi mkuu ujao wa Agosti 9.