"Nikiwa mbunge nitapeleka mswada wa matibabu ya Endometriosis" - Fyah Mummah

Njambi amekuwa akisumbuliwa na Endometriosis kwa muda mrefu na aliahidi akiwa mbunge atawasilisha mswada wa kunufaisha wanawake wenye hali hiyo.

Muhtasari

• “Kunio natabasamu ni furaha. Kuniona nikisimama ni kazi ya Mungu. Kuona mimi napiga kampeni ni muujiza kwamba Mungu hurejesha watu,” alisema Njambi.

Mwaniaji ubunge Dagoretti kusini Mary Njambi Koikai
Image: Fyah Mummah Jahmby Koikai (Facebook)

Mwaniaji wa ubunge Dagoretti Kusini mtangazaji Mary Njambi Koikai anayefaamika na wapenzi wengi wa muziki wa Reggae kama Fyah Mummah Jahmby ametoa ahadi ya kupigania haki za kina dada haswa wenye matatizo ya hedhi kwa lugha ya kimombo Endometriosis, pindi atakapoteuliwa kama mbunge.

Mwanadada huyo ambaye analenga kuwa mbunge kama mgombea huru amekuwa kwa muda mrefu akipigana vita na tatizo hilo ambalo limemsumua tangu utoto wake ambapo ametafuta msaada si haba ili kufanyiwa upasuaji kwa ajili ya kutibu tatizo hilo.

Akiandika kupitia ukurasa wake wa Facebook, Njambi alisema kwamba ni kwa muujiza wa Mungu kumuona tena anatabasabu na kusimama hadi kushiriki katika kampeni za kujipigia debe kuelekea uchaguzi wa Agosti 9.

“Kunio natabasamu ni furaha. Kuniona nikisimama ni kazi ya Mungu. Kuona mimi napiga kampeni ni muujiza kwamba Mungu hurejesha watu,” aliandika Njambi.

Akionekana kutumia tatizo hilo lake la kiafya kunadi sera zake, Njambi alisema kwamba kuna mamilioni ya wanawake humu nchini ambao wanapigana vita vya kisiri na tatizo la Endometriosis na Adenomyosis na hivyo kuahidi kwamba pindi atakapochaguliwa kwenda bungeni atapigania haki za wanawake kama hao kupata matibabu yanayofaa na pia kutenga fedha zaidi za kufanya utafiti kuhusu tiba ya tatizo hilo sugu.

“Kuna mamilioni ya wanawake katika nchi hii wanaopambana na Endometriosis na Adenomyosis. Kwa kuchaguliwa kwangu bungeni, nakusudia kutunga na kutunga sera zitakazowezesha wasichana na wanawake kupata matibabu bora, madaktari wetu wa magonjwa ya wanawake kupewa mafunzo maalum ya upasuaji wa kushughulikia matatizo hayo, kutenge fedha zaidi kutafiti ugonjwa huu mbaya,” alisema Njambi.

Njambi ni mtangazaji mmoja miongoni mwa wengi ambao wamejitosa ulingoni kuwania nyadhifa mbalimbali za kisiasa katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9. Watangazaji wengine ni pamoja na Phelix Odiwuor almaarufu Jalang’o anayelenga ubunge Lang’ata, Boniface Musambi anayelenga ubunge Kitui ya Kati miongoni mwa majina mengine makubwa kwenye tasnia ya Uanahabari na mawasiliano.

Njambi analenga kumng’atua mamlakani mbunge wa sasa John Kiarie ambaye pia analenga kukitetea kiti hicho kwa tikiti ya chama cha UDA,  huku akikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mbunge wa zamani Dennis Waweru anayelenga kurudi tena kwa tikiti ya Jubilee.