Pigo kwa Wanjigi baada ya Mahakama kuu kutupilia mbali kesi kuhusu kibali cha IEBC

Muhtasari
  • Kulingana na Wanjigi, jinsi alivyofutiliwa mbali katika orodha ya mgombea urais ilitia shaka
  • Kulingana na Wanjigi, Kamati ya Kusuluhisha Mizozo ya IEBC ilikosea kisheria kutupilia mbali malalamishi yake
Jimi Wanjigi
Jimi Wanjigi
Image: EUTYCAS MUCHIRI

Mahakama Kuu imetupilia mbali ombi lililowasilishwa na mgombea urais wa Chama cha Safina Jimi Wanjigi akitaka jina lake lijumuishwe katika orodha ya wagombeaji urais katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Jaji Jairus Ngaah alitupilia mbali ombi hilo kwa msingi kwamba Wanjigi alikosa kuwasilisha kesi ya lazima mbele ya mahakama kuhusu ni kwa nini jina lake linastahili kupigwa kura.

Wanjigi aliwasilisha ombi hilo baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kukataa ombi lake la kuidhinishwa kuwania urais mwezi Agosti kwa kukosa shahada ya chuo kikuu. Alikuwa akiitaka mahakama kufutilia mbali uamuzi wa IEBC na kuamuru mwenyekiti Wafula Chebukati amteue kuwa mgombeaji urais.

Kulingana na Wanjigi, Kamati ya Kusuluhisha Mizozo ya IEBC ilikosea kisheria kutupilia mbali malalamishi yake.

"Agizo la Mandamus likimuelekeza Chebukati kujumuisha jina la Jimi Wanjigi kwenye karatasi za kura kwa uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika Agosti 9," ombi la Wanjigi linatafuta kwa sehemu.

Wanjigi amemkashifu Chebukati kwa kumnyima faida pakubwa yeye na kampeni yake baada ya kukosa kumwidhinisha kuwania  uchaguzi wa Agosti.

Kulingana na Wanjigi, jinsi alivyofutiliwa mbali katika orodha ya mgombea urais ilitia shaka.