Tingiza mti: Wajackoyah asema Kenya itauzia Wachina korodani za fisi, ni dawa kwao

Wajackoyah akizindua manifesto yake alisema Kenya itauzia Uchina korodani za fisi, nyama ya mbwa na nyama ya nyoka.

Muhtasari

• “Tutauza nyama ya fisi kwa Uchina, kwa sababu sisi hatuhitaji fisi katika Kenya hii." - Wajackoyah

Profesa George Wajackoyah
Image: Youtube (Sceenshot)

Mwaniaji wa kiti cha urais wakili msomi profesa George Wajackoyah Alhamisi usiku alizindua manifesto yake rasmi kwa umma kutoka ukumbi wa KICC.

Miongoni mwa masuala tete ambayo Wajackoyah aligusia kwenye manifesto yake na ambayo yamezua gumzo kubwa sana kwenye mitandao ya kijamii ni kuahidi kwamba akiwa rais atahakikisha ameimarisha uhusiano wa kibiashara na Uchina.

Katika manifesto yake, Wajackoyah alionekana kuzungumzia mambo mengi tu yanayolenga nchi ya Uchina ambapo kando na awali kusema kwamba atahalalisha ufugaji wa nyoka ili kuuzwa kwa wachina kama Chakula, pia alisema kwamba tutafuga mbwa na kuwauzia Wachina kama nyama.

Msomi huyo sasa amezua gumzo tena baada ya kusema kwamba Kenya itauzwa korodani za fisi kwa Wachina na kusema kwamba Wachina wanapenda nyama hiyo.

“Tutauza nyama ya fisi kwa Uchina, kwa sababu sisi hatuhitaji fisi katika Kenya hii. Mchina anakula fisi.” Alisema Wajackoyah.

Msomi huyo wa sheria aliendelea mbele kudadavua zaidi suala hilo ambapo alitoa takwimu kwamba Kenya kuna fisi zaidi ya elfu na kila fisi ana korodani mbili, na hizo takwimu zikijumuishwa vizuri Kenya itavuna pakubwa kutokana na biashara ya kuuza korodani za fisi nchini Uchina.

“Mimi nasikia fisi elfu moja wa kiume, wako na korodani elfu mbili. Na mimi nasikia hizo korodani ni dawa kwa Uchina. Hizo korodani ni za gharama kubwa zaidi kushinda hata Ganja. Korodani moja ni karibu milioni sita. Kwa hiyo tutauza Uchina korodani za fisi, nyama ya mbwa na nyama ya nyoka.” Alisema Wajackoyah huku umati uliokuwa umefurika kwenye ukumbi wa KICC ukimshangilia kwa kelele zisizojua kikomo.

Profesa Wajackoyah pia alizidi kudadavua zaidi kwamba gharama ya bei ya mbwa iko juu zaidi kuliko hata nyama ya mbuzi na ng’ombe ambazo taifa la Kenya linauza nje ya nchi.

“Kilo moja ya nyama ya mbwa inauza mara sita zaidi ya bei ya nyama ya mbuzi kilo moja. Kenya inauza nje nyama ya mbuzi na ng’ombe kule Mashariki ya kati. Kwa hiyo acha nisisitize hapo tena, nyama ya nyoka inaenda Uchina, wakishakula, deni tumelipa.” Alisisitiza Wajackoyah.