Sijakuomba uniunge mkono!- DP Ruto amjibu rais Kenyatta

Muhtasari

•Ruto alimkashifu Rais akisema hajamwomba uungaji mkono na kuongeza kuwa yuko tayari kukabiliana na Raila.

•Uhuru alisema DP alikuwa na miaka minane ya kutekeleza ahadi nyingi za maendeleo anazotoa sasa lakini hakuweza.

DP RUTO WAKATI WA MANIFESTO YA KENYA KWANZA 30 JUNI 2022
Image: EZEKIEL AMING'A

Naibu Rais William Ruto amemsuta bosi wake Uhuru Kenyatta dakika chache tu baada ya kumwambia kuwa "ameshindwa kutekeleza majukumu yake".

Akizungumza katika mji wa Chuka, Kaunti ya Tharaka Nithi, Naibu Rais alimtaka Rais aondoke kwenye siasa kwani hagombei urais.

Alimkumbusha bosi wake kuwa mchuano huo ni kati yake na kinara wa ODM Raila Odinga.

Ruto alimkashifu Rais akisema hajamwomba uungaji mkono na kuongeza kuwa yuko tayari kukabiliana na Raila ana kwa ana na kumshinda katika uchaguzi wa Agosti 9.

"Si munisaidie tuambie Uhuru Kenyatta awache nishindane na bwana Kitendawili. Ama niaje, si aniwachie nipambane na Raila?"  Alisema siku ya Jumamosi.

"Na mimi sijamuambia Uhuru Kenyatta anisupport, wacha akae kando. Mimi ni mzuri kutosha. Huyu kitendawili nitamumalizia asubhi na mapema."

Matamshi ya DP yalikuja baada ya Uhuru kumshutumu kwa kutoa ahadi tupu lakini alikuwa na wakati wa kutimiza kile anachoahidi Wakenya.

Akizungumza katika hafla iliyofanyika KICC Jumamosi, Rais bila kutaja jina lake, alimsuta naibu wake kwa kutoa ahadi nyingi ilhali alikuwa na fursa ya kutekeleza.

Uhuru alisema DP alikuwa na miaka minane ya kutekeleza ahadi nyingi za maendeleo anazotoa sasa lakini hakuweza.

"Nasikitika nikiona wengine huko ng'we ng'we. Mtu amepewa kazi, badala ya kazi ni mdomo, mdomo, mdomo tu. Alafu anaanza kusema tutafanya na tutafanya," alisema.

"Kwa nini haukufanya ukiwa na kazi.Hii maneno ya makelele huko, huko, watu wawache upuzi... Munya hapa amefanya kazi kwa miaka mitatu. Hao walikua miaka nane walifanya nini?"

Aliongeza:

"Wakiona mtu na shida wanasema watatatua. Kwa nini hamkutatua mkiwa ofisini?"

Rais aliendelea kuwahimiza Wakenya kufanya maamuzi ya busara kabla ya uchaguzi wa Agosti huku akiwakumbusha mustakabali wao uko hatarini.