Agnes Kagure: Napunguza kasi ya kampeni ili wanifikie, sitaki kuwashinda sana!

Kagure aliamua kuwania ugavana kama mgombea huru baada ya Jubilee kumnyima tikiti.

Muhtasari

• Agnes kagure anadai yeye ni maarufu zaidi ya Sakaja na Igathe na kwamba atapunguza mbio za kampeni ili asiwaache sana.

Mwaniaji wa ugavana Nairobi, Agnes Kagure
Mwaniaji wa ugavana Nairobi, Agnes Kagure
Image: Twitter

Mwaniaji wa ugavana katika kaunti ya Nairobi, Agnes Kagure amegeuzwa gumzo la mtandao wa Twitter baada ya kuibua madai kwamba yeye ndiye anayeongoza katika tafiti mbali mbali zinazoonesha washiriki katika mbio za kuelekea City Hall.

Kagure kupitia mtandao wake wa Twitter alisema kwamba ako mbele sana na sasa anafikiria kupunguza kasi yake ili wapinzani wake angalau wamkaribie kwa sababu kulingana na yeye, hakuna mwaniaji mwingine wa ugavana anayemkaribia kwa umaarufu.

Kagure alisema kwamba huruma zake zimemtuma kufikiria kuwapa wapinzani wake nafasi kidogo ya kumkaribia ili kuwanusuru kutokana na aibu kwa sababu hataki kuwashinda sana.

“Sasa ninafikiria kupunguza kasi ya kampeni zangu ili kuwapa washindani wangu nafasi ya angalau kunikaribia katika umaarufu na kusitiri nyuso zao kutokana na aibu. Sitaki kuwashinda sana,” Kagure aliandika kwenye Twitter.

Image: Twitter

Ujumbe huu ulikuja kwa njia fulani hivi kama utani kwa watu wengi ambao walimwambia kwamba tafiti ambazo zimefanywa na kampuni mbalimbali zinaonesha umaarufu mkubwa upo katika wagombea wawili wakuu wanaolinganishwa kama farasi na kumwambia kwamba yeye labda kama hajakuwa katika kundi la punda basi atakuwa kwenye safu ya vihongwe katika mbio hizo.

Tafiti mbali mbali ambazo zimekuwa zikitolea kila mwezi na kampuni kadhaa zinaonesha ushindani upo kati ya Johnson Sakaja wa chama cha UDA na Polycarp Igathe wa Jubilee.

Kagure anawania ugavana Nairobi kama mgombea huru baada ya chama cha Jubilee kumnyima tikiti na badala yake kumkabidhi Polycarp Igathe.

Muungano wa Azimio-One Kenya uliwataka wagombea mbali mbali kutupilia mbali azma zao za kutaka kuwania viti mbali mbali na kuwaunga mkono wenzao walioonekana kuwa na ufuasi mkubwa, ambapo awali chama cha Jubilee kilikuwa na wagombea kadhaa akiwemo mfanyibiashara Richard Ngatia ambaye alikubali kuachia ila Kagure akajitetea na kusema kwamba katu hawezi kuwafeli mamia ya watu wanaomtegemea kuleta ukombozi City Hall.