Mgombea mwenza wa mwaniaji ugavana Kisii ajiuzulu na kujiunga na mpinzani wake

Dkt. Alfred Ndemo alikuwa ameteuliwa kama mgombea mwenza wa Manson Nyamweya kuwania ugavana wa chama cha KNC.

Muhtasari

• Dkt. Ndemo alijiuzulu na kujiunga na kambi ya Simba Arati ambaye pia anawania ugavana.

• Nyamweya alisema hilo halibadilishi chochote kando na kuipoteza ile kura yake moja.

Aliyekuwa mgombea mwenza wa Manson Oyongo Nyamweya kaunti ya Kisii
Aliyekuwa mgombea mwenza wa Manson Oyongo Nyamweya kaunti ya Kisii
Image: Kisii Hot (Facebook)

Dkt. Alfred Ndemo, mgombea mwenza wa mwaniaji ugavana kaunti ya Kisii Manson Oyongo Nyanweya amejiuzulu wadhifa huo na badala yake kujiunga na kundi la Simba Arati ambaye pia anawania ugavana wa kaunti hiyo.

Katika taarifa zilizozagaa Jumatano alasiri, Dkt. Ndemo alibwaga manyanga kuwa mgombea mwenza wa Nyamweya wa KNC na kujiunga na mpinzani wake mkuu Simba Arati wa ODM ambaye alikuwa mbunge wa Dagoretti Kaskazini.

Haya yanatokea tu siku chache baada ya Nyamweya kuonekana kwenye mkutano wa kisiasa akiwatukana baadhi ya viongozi wakubwa kutoka eneo hilo huku akiwadhalilisha kuwa wao ni watoto wadogo wanafaa kunyamaza wakati anazungumza.

Maneno hayo yake yalionekana kulenga kundi la Arati ambaye anaungwa mkono na Waziri wa usalama wa ndani Dkt. Fred Matiang’i.

Taarifa za kutorokwa na mgombea mwenza wake zilimpata Nyamweya kwa ghafla kama chafya ambapo aliita mkutano wa habari na kusema kwamba hilo halimstui kwani atakuwepo kwenye debe katika uchaguzi ujao.

“Siku ya leo nimesikia kutoka vyombo vya habari kwamba mgombea mwenza wangu ameachia ngazi na kujiunga na mpinzani wangu. Hilo halina tatizo hata kama ameenda kitu tu nitakosa ni hiyo kura yake moja, lakini jina lake litasalia kwenye karatasi za kupiga kura pamoja na langu,” Nyamweya alisema kwa wasiwasi mkubwa.

Manson Nyamweya ambaye kwa wakati mmoja alikuwa mbunge wa Mugirango ya Kusini analenga kuwa gavana wa pili wa kaunti hiyo yenye utajiri wan dizi ila sasa safari yake ya kumrithi gavana Ongwae imebaki kwenye njia panda akiwa amebaki bila mgombea mwenza mwezi mmoja tu kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.