Ruto: Uhuru alikataa Maaskofu wasitupatanishe, nimemvumilia sana, amekuwa akinidhalilisha

Ruto alisema yeye ni mwenye subira na angekuwa ni mtu mwingine anafanyiwa vile yeye anafanyiwa na Kenyatta, mambo yangekuwa mabaya.

Muhtasari

• "Uliza maaskofu, uliza Askofu wa ACK, Uhuru alikataa tusipatanishwe” - Ruto

Naibu rais na kiongozi wa Kenya Kwanza
Naibu rais na kiongozi wa Kenya Kwanza
Image: William Samoei Ruto (Facebook)

Hatimaye, naibu wa rais William Ruto amezungumzia kilichotokea baina yake na bosi wake rais Uhuru Kenyatta mpaka kupelekea urafiki wao uliokuwa umeshuhudiwa bayana tangu mwaka 2013 kuzorota na wawili hao kuanza kutupiana mabomu mazito ya maneno.

Akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na kituo kimoja cha runinga humu nchini katika ukumbi wa mgahawa wa Serena jijini Nairobi, Ruto alielezea kwamba rais Uhuru Kenyatta ndiye mwenye kulaumiwa kwa kuzorota kwa urafiki wao kwani hata maaskofu walijaribu kuwapatanisha lakini Kenyatta akakataa na kuchagiza zaidi uhasama wao.

“Kwa kweli ni kwa bahati mbaya sana na ninajuta pakubwa kwa sababu ni moja kati ya vitu ambavyo sikuwa navitegemea kabisa kukosana na bosi wangu. Acha niseme ukweli, nimekuwa mtu mwenye Subira sana. Kule kudhalilishwa ambako nimeoneshwa kutoka kwa bosi wangu, hakuna mtu mwingine angeweza kustahimili,” alisema Ruto.

Kinara huyo wa muungano wa Kenya Kwanza pia alisema kwamba dharau ambazo Uhuru Kenyatta amemuonesha wangekuwa ni wengine kama Raila au Martha Karua, mambo yangekuwa mabaya sana ila kwa sababu yeye ni mwenye Subira, amejitahidi sana muda mrefu kutojibizana na mkubwa wake, Uhuru Kenyatta.

Aidha, Ruto alipuuzilia mbali madai yanayosemekana kwamab amewahi mdhalilisha Uhuru na kusema kwamab yeye mwenyewe alikuwa na mazungumzo na Kenyatta ambapo alimtaka atoe Ushahidi wa video inayoonyesha kwamba amemdhalilisha lakini rais Kenyatta akakana kwamba hakuna kitu kama hicho.

“Maaskofu walizungumza na mimi, wakaenda wakazungumza na rais Kenyatta na waliporejea kwangu niliwaambia nataka watupatanishe na Kenyatta, lakini yeye alikataa. Uliza maaskofu, uliza Askofu wa ACK,” Ruto alitema ukweli.

Akizungumzia madai ya kutaka kumzaba kofi rais, Ruto alisema kwamba ile ilikuwa lugha ya kimafumbo tu na ambayo sasa wapinzani wake wa kisiasa wanaitumia nje ya muktadha halisi.