Raila alipanga kesi ya Uhuru na Ruto ICC, Seneta Kindiki adai

Alisema ni ‘usaliti wa hali ya juu’ kwa Rais Kenyatta kumtupa nje ya serikali Dkt Ruto

Muhtasari

•Alisema Mkuu wa Nchi pia hana shukrani kwa sababu Dkt Ruto alimsaidia kushinda mara mbili "na sasa anampigia kampeni Bw Odinga waziwazi."

•Seneta huyo aliwataka wakazi hao "kumwaibisha" Uhuru kwa kumpigia kura nyingi Dkt Ruto katika uchaguzi wa Agosti 9.

Seneta wa Tharaka Nithi Kithure Kindiki
Image: Andrew Kasuku

Seneta wa Tharaka Nithi Kithure Kindiki amemshutumu mgombea urais wa Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga kwa kupanga kesi ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Hii ilikuwa baada ya ghasia zilizoshuhudiwa Kenya mwaka wa 2007 na 2008 baada ya Rais wa zamani Mwai Kibaki kutangazwa mshindi wa uchaguzi mkuu uliofanyika Desemba 27, 2007.

Akizungumza katika soko la Kibunga eneo bunge la Tharaka Jumapili, Prof Kindiki ambaye aliandamana na Spika Justin Muturi na Gavana wa Tharaka Nithi Muthomi Njuki alisema Bw Odinga alipanga njama na baadhi ya watu wa nje kutaka Mkuu wa Nchi na naibu wake wafungwe jela.

Alisema ni ‘usaliti wa hali ya juu’ kwa Rais Kenyatta kumtupa nje ya serikali Dkt Ruto na washirika wake waliosimama naye wakati wa mivutano ya ICC na kumkaribisha mpinzani wake, Bw Odinga.

"Inashangaza na tena usaliti mkubwa kuona Rais Kenyatta akimkumbatia na kumuunga mkono Bw Odinga ambaye alikuwa amepanga njama ya kumfikisha mahakamani katika mahakama ya ICC," Prof Kindiki alisema.

Alisema Mkuu wa Nchi pia hana shukrani kwa sababu Dkt Ruto alimsaidia kushinda mara mbili "na sasa anampigia kampeni Bw Odinga waziwazi."

Seneta huyo aliwataka wakazi hao "kumwaibisha" Uhuru kwa kumpigia kura nyingi Dkt Ruto katika uchaguzi wa Agosti 9.

Pia alipigia debe uungwaji mkono kwa wagombeaji wa Ugavana Njuki ambaye anatumia tiketi ya  UDA akiteta kuwa itakuwa mbaya kumpigia kura Dkt Ruto na kuwachagua wawaniaji kutoka vyama vingine.

Bw Muturi aliwahakikishia wakazi wa Mlima Kenya Mashariki kwamba kwa kuwepo kwa Prof Kindiki Kenya Kwanza, maslahi yao yatashughulikiwa iwapo Dkt Ruto atashinda urais katika uchaguzi wa Agosti 9.

Alisema Kenya haiwezi kushurutishwa na Rais Kenyatta kumpigia kura Bw Odinga kwa sababu hana ajenda ya kuboresha uchumi.

Alisema Dkt Ruto ameeleza mipango yake ya kuboresha uchumi na kwamba ana uwezo wa kutekeleza.