Raila anaongoza dhidi ya Ruto katika kinyang'anyiro cha urais - Kura ya maoni

George Wajackoyah yupo katika nafasi ya tatu akiwa na uungwaji mkono wa 4%.

Muhtasari

•Asilimia 42 ya wapiga kura wanamuunga mkono Raila ikilinganishwa na asilimia 39 waliosema watampigia kura William Ruto. 

• George Wajackoyah wa Roots Party yupo katika nafasi ya tatu akiwa na uungwaji mkono wa 4%.

Raila Odinga
Mgombea urais Raila Odinga Raila Odinga
Image: RAILA ODINGA/TWITTER

Mgombea urais wa Azimio-One Kenya Raila Odinga atamshinda mpinzani wake mkuu William Ruto katika kinyang'anyiro cha urais iwapo uchaguzi ungefanyika hivi leo, utafiti mpya unaonyesha.

Matokeo ya Trends and Insights Africa (TIFA) yanaonyesha kuwa asilimia 42 ya wapiga kura wa Kenya wanamuunga mkono Raila ikilinganishwa na asilimia 39 waliosema watampigia kura William Ruto. 

"Raila ana asilimia 3 ya ushindi dhidi ya Ruto," Tom Wolf, Mtafiti Mkuu wa Tifa alisema.

Kura ya maoni ilikuwa na ukingo wa makosa wa +/- 2.34.  Kitaalamu hii inamaanisha kuwa nchi itashiriki duru ya pili ya uchaguzi huo kwa kuwa hakuna mgombea yeyote kati ya wawili hao maarufu zaidi ambaye angevuka alama 50+1.

Hata hivyo, asilimia 10 ya waliohojiwa walisema kuwa bado hawajaamua ikiwa imesalia siku 28 kabla ya uchaguzi.  

Ripoti iliyotolewa Jumatatu pia inamuorodhesha George Wajackoyah wa Roots Party katika nafasi ya tatu akiwa na uungwaji mkono wa 4%.

Utafiti huo uliofanyika kati ya Juni 25 hadi Juni 30  na kuwashirikisha wahojiwa 1,533 kutoka mikoa tisa nchini kote.

(Utafsiri: Samuel Maina)