'Kwetu hatuwachapi wanawake kofi,'DP Ruto ajibu madai ya waziri Wamalwa

Matamshi ya Naibu Rais yanajiri baada ya Waziri Wamalwa kumshutumu kwa nusura apige makofi katika mkutano wa hadhara Kakamega Ijumaa iliyopita.

Muhtasari
  • Naibu Rais William Ruto amemkashifu waziri wa ulinzi Eugene Wamalwa kwa kukosa shukrani
Naibu rais na kiongozi wa Kenya Kwanza
Naibu rais na kiongozi wa Kenya Kwanza
Image: William Samoei Ruto (Facebook)

Naibu Rais William Ruto amemkashifu waziri wa ulinzi Eugene Wamalwa kwa kukosa shukrani.

Ruto ambaye alizungumza Trans Nzoia wakati wa ziara yake ya kampeni aliteta kuwa licha ya kumsaidia kupata wadhifa wa baraza la mawaziri katika serikali ya Jubilee, waziri huyo amemgeuka.

DP, ambaye alikuwa akimjibu Wamalwa kuhusu madai yake ya hivi majuzi kwamba alikaribia kumpiga kofi, alimkemea akisema "Katika jamii yetu, hatupigi wanawake makofi, tunawaheshimu."

Alisema Wamalwa ambaye ameungana na wapinzani wake sasa hangekuwa na kazi kama si yeye.

"Mwambie huyo mjamaa awache kuongea mingi, bila mimi angekuwa anatembea kwa barabara, mimi ndiye nilimtoa kwa mtaro na nikampatia kazi ya waziri. Serikali mimi ndiye niliunda na Uhuru Kenyatta huyo jamaa alikuwa anahangaika kwa barabara, unaongea kama nani? Bure kabisa."

Matamshi ya Naibu Rais yanajiri baada ya Waziri Wamalwa kumshutumu kwa nusura apige makofi katika mkutano wa hadhara Kakamega Ijumaa iliyopita.

"Nataka kukuambia leo kwamba hata mimi Eugene Wamalwa mwanao, karibu nipigwe kofi na jamaa huyo. Aliniambia nitoke nje ya serikali yake na kunikabidhi barua ya kujiuzulu siku iliyofuata," alisema.