Afueni kwa Sonko, IEBC yaamrishwa kumjumuisha kwenye kinyang'anyiro cha ugavana Mombasa

IEBC ilikuwa imemzuia Sonko kuwania kwa madai kwamba kesi yake ya kung'atuliwa mamlakani haikuwa imekamilika

Muhtasari

• Mahakama kuu imetupilia mbali hatua ya IEBC kumzuia kuwania ugavana Mombasa.

Aliyekuwa gavana wa Nairobi, Mike Sonko
Aliyekuwa gavana wa Nairobi, Mike Sonko
Image: Facebook

Ni ushindi mkubwa kwa aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko baada ya mahakama kuu kufutilia mbali hatua ya tume  huru ya uchaguzi na mipaka IEBC kumfungia nje ya kinyang'anyiro cha ugavana wa Mombasa

IEBC pia imeagizwa kuchapisha jina la Sonko kwenye gazeti la serikali. Mahakama iliamua kwamba IEBC na CRO walifanya visivyofaa kumzuia Sonko kuwa kwenye kinyang'anyiro hicho.

Jopo la majaji watatu wakiongozwa na  Olga Sewe, Ann Ong'injo' na Stephen Githinji walitoa uamuzi huo siku ya Jumatano asubuhi na kusema kwamba tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC  pamoja na afisa wa CRO walienda kinyume na sheria kumzuia Sonko kuwania wadhifa wa gavana wa Mombasa.

Jopo hilo lilitaka IEBC kujumuisha jina la Sonko na mgombea mwenza wake Ali Mbogo kwenye karatasi za kupiga kura kaunti ya Mombasa.

"Kwa hivyo, ombi hilo linaruhusiwa na maombi kukubaliwa, na mshitakiwa wa tatu (IEBC) anaelekezwa kukubali karatasi za uteuzi zilizowasilishwa na mlalamishi (Sonko),” uamuzi wa jopo huo ulisema.

Sonko analenga kumrithi gavana wa kwanza wa kaunti hiyo ya pwani Ali Hassan Joho kupitia tikiti ya chama cha Wiper.

Awali, kulikuwa na taarifa kwamba baada ya chama hicho kuona kwamba huenda Sonko hangeruhusiwa kugombea, walikuwa wamewasilisha jina la Ali Mbogo kama mgombea na badala yake Mike Sonko kuwa mgombea mwenza, kama njia moja ya kuhakikisha chama hicho hakingefungiwa nje kutoa mgombeaji.