Mudavadi adai kuwa kura za maoni zinatumika kuhadaa wananchi kuunga mkono Azimio

Amesema Azimio ikiongozwa na Uhuru na Kibaraka wake Raila Odinga, wamekataliwa na wakenya kutokana na uendeshaji mbaya wa serikali

Muhtasari

• Mudavadi alisema kuwa hakuna kurudi nyuma tena kwani kipenga cha uchaguzi wa Agosti tisa kishapulizwa.

Kinara wa ANC Musalia Mudavadi
Kinara wa ANC Musalia Mudavadi
Image: WILFRED NYANGARESI

Kinara wa Chama cha ANC Musalia Mudavadi amejiunga na wenzake kwenye mrengo wa Kenya Kwanza Kushtumu vikali mwelekeo ambao anadai unachukuliwa na wapinzani wao wa Azimio kwa kukashifu vikali matumizi ya kura za maoni kuwahadaa wakenya kuwa Azimio ina umaarufu wa juu kuliko Kenya Kwanza.

Mudavadi akizungumza kwenye mahojiano na kituo kimoja cha radio cha humu nchini amezidi kukosoa wapinzani wao wakuu kutoka mrengo wa Azimio kwa kuanzisha mijadala inayoonekana kuegemea katika kupinda mkondo uliowekwa wa maandalizi ya uchaguzi na tume huru ya Uchaguzi na Uratibu wa Mipaka nchini, IEBC. Akirejelea hotuba yake akiwa kwenye kampeni za Kenya Kwanza wikendi iliyopita Mudavadi ameelezea kuwa hata ile kura ya maoni iliyotolewa siku ya Jumatatu ya shirika la utafiti la TIFA, ni ishara tosha kuwa kuna ushirikiano wa karibu wa mashirika hay ana usimamizi wa Azimio ambao kwa sasa upo kwenye hali ya wasi wasi.

“Azimio which is ODM has started showing signs of panic. They should not try and intimidate the IEBC or give IEBC conditions. The Law that is there is for all candidates and all Kenyans. You cannot try to change the law at this hour. Kwa hivyo muache kutoa vitisho kwa IEBC, muache kuambia watu mtasusia, hii mambo ya kusema mtasusia ni dalili ya kuonyesha kwamba zile opinion polls mmekuwa mkitoa za uwongo ati nyinyi mko mbele mmenza kuona dalili kwamba mtashindwa asubuhi na mapema.” ~ H.E Musalia Mudavadi.

Mudavadi amesisitiza kuwa wakati sasa umewadia kwa wakenya kufanya uamuzi wa busara na wa kina kuhusiana na mwelekeo ambao wanaitaka nchi hii iuchukue.

Mudavadi alisema kuwa hakuna kurudi nyuma tena kwani kipenga cha uchaguzi wa Agosti tisa kishapulizwa na sasa pande zote kinzani hasa kwenye kinyang’anyiro cha ikulu ni sharti kijizatiti kuona kuwa kinafika utepeni.

“Sisi tunasema kwamba uamuzi uwe pale na wale ambao wamegusia mambo ya kususia uchaguzi tusirudi huko, it is decision time. Hatuwezi tukafika wakati wa kura na tena tunaanza kugusia mambo ya kususia uchaguzi. We have to make a decision.” ~ H.E Musalia Mudavadi.

Ikiwa zimesalia tu siku 26 kabla ya wakenya kufika kwenye debe kushiri zoezi hili linalodhihirisha haki yao ya kikatiba na kidemokrasia, Mudavadi amesema kuwa upande wa Azimio umeanza kutoa vitisho baridi kwa tume ya IEBC na kuibua masuala ambayo hayana msingi wowote kuambatana na maandalizi ya uchaguzi.

Amesema kuwa Azimio ambayo kinara wake ni Rais Uhuru Kenyatta na Kibaraka wake Raila Odinga, wamesahau kuwa wakenya wamewatema kutokana na uendeshaji mbaya wa serikali ambao umechangia pakubwa kuzorota kwa uchumi, kukopwa kwa madeni makubwa makubwa ya umma, ongezeko la bei za bidhaa muhimu kama vile unga, mafuta ya kupika, mafuta taa, petroli na ukosefu wa ajira na mapato ya kilimo kutokana n akule kuwatelekeza wananchi ambao sasa wengi wao wamezamia kwenye lindi la taabu na umaskini.

“Bei ya Chakula hairuki tu. Inaruka kwa sababu madeni ni mazito kwa sababu ya wale walio mammlakani wametuweka ndani, na kwa sasa tuko kwa shimo na njia fupi ya kutoka kwa shimo ni kuwacha kuchimba. Tarehe tisa mwezi Agosti ni lazima tukome kuchimba hilo shimo ili lisiende zaidi.” ~ H.E Musalia Mudavadi.

Mudavadi akiupigia debe mrengo wa Kenya Kwanza kwa kusema kuwa sera zinazotokana na manifesto ya Kenya Kwanza ni sera ambazo zinamlenga mwananchi wa kawaida hasa kutokana na utafiti walioufanya kupitia wataalam wao. Mudavadi akirejelea suala la kupiga jeki kilimo hasa kwa kupunguza bei ya mbolea na pembejeo, kuimarisha ukuzaji kwa kuwapa wakulima mapato na kuwaelimisha kupitia mbinu za kisasa zitakazosaidia kuongeza uzalishaji kama vile kwenye ukulima wa ng’ombe wa maziwa pamoja na kurejesha ule mfumo wa kuwepo kwa maafisa wa kilimo watakaokuwa wakitoa mafunzo kwa wakulima maeneo tofauti tofauti ya nchi.