Nelson Havi wa UDA aonekana kumpigia debe Igathe wa Azimio, apakia manifesto yake

Nelson havi anawania ubunge Westlands kwa tikiti ya UDA, ambacho ni chama cha William Ruto.

Muhtasari

• Nelson Havi anayeegemea mrengo wa naibu rais William Ruto kwa mara nyingine ameonekana kumpigia debe mgombea wa muungano pinzani, Azimio-One Kenya.

• Waakti fulani pia aliwahi msifia Martha Karua kuwa mgombea mwenza bora huku maswali yakiibuliwa kama kweli yuko Kwa Ruto ama kwa Raila.

Wakili ambaye pia anagombea ubunge Westlands, Nelson Havi
Wakili ambaye pia anagombea ubunge Westlands, Nelson Havi
Image: Facebook

Wakili na ambaye aliwahi kuhudumu kama rais wa awamu ya 49 wa chama cha wanasheria wa humu nchini Nelson Havi kwa mara nyingine amewaacha wafuasi wake katika njia panda baada ya kupakia picha ya kitabu cha manifesto ya mgombea ugavana wa Nairobi kutoka muungano wa Azimio-One Kenya, Polycarp Igathe.

Hili linawachanganya wafuasi wake haswa ikizingatiwa kwamba Havi ambaye anawania ubunge Westlands kupitia chama cha UDA, ambacho ni mpinzani mkubwa wa Azimio-One Kenya ni kama mahasimu wawili wa kisiasa.

“Polycarp Igathe amefanya tena. Ameleta gazeti nyumbani kwangu,” Havi alifuatisha na ujumbe huo katika picha ya manifesot ya Igathe aliyoipakia.

Baadhi wanadai mwanasheria huyo msomi anaonekani kumpigia debe Igathe ambaye anawania kutoka mrengo pinzani na ule mrengo ambao yeye yupo na hili linazidi kuwachanganya wafuasi wake ambao hawajui iwapo kweli Havi yupo nyuma ya Raila ama yupo nyuma ya Ruto.

Hii si mara ya kwanza Havi analeta utashi mitandaoni kwani itakumbukwa mara baada ya martha Karua kuteuliwa kama mgombea mwenza wa Raila, Havi alimmiminia sifa na kumvisha koja la maua huku akisema kwamba maam huyo ni chaguo bora.

Wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wanahisi Havi hafurahishwi na Sakata linaloendelea kwamba mgombea ugavana Nairobi kupitia chama cha UDA, Johnson Sakaja kwamba hana digrii ya kweli na ndio maana hata siku moja hajasikika ama kuonekana akimpigia debe ilhali anamnadi Igathe ambaye ni mpinzani wao.

“Mimi nafikiri bwana Havi ungebakia tu kwenye kuwakilisha wateja wako katika kesi maana unaonekana hujielewi kabisa kuhusu yule unayemuunga mkono, naamini una uhakika kuhusu hasira za bosi wako chunga usije ukapata kofi pia,” mmoja kwa jina Charles Mac’Adhola aliandika.

Wengi walichukulia hili kama Havi ambaye ni wa mrengo wa naibu rais, anawapigia debe wagombea wa mrengo pinzani hali ya kuwa katika nafasi hiyo, mrengo wake bado una wagombea.