Serikali haina mpango wa kuvuruga uchaguzi wa Agosti-Kibicho

Alisema kukutana na machifu ni hatua ya kawaida ambayo ipo chini ya mamlaka yake

Muhtasari

•Alisema kukutana na machifu na wasimamizi wengine ni masuala ya kawaida ya usalama ambayo yako chini ya mamlaka yake.

•Pia alitetea kamati ya mpito iliyoundwa hivi majuzi akisema rais ameagizwa na sheria kuunda kamati ya dhana ya kusimamia mpito.

Waziri wa mambo ya Ndani Karanja Kibicho.
Waziri wa mambo ya Ndani Karanja Kibicho.
Image: STAR

Katibu Mkuu katika wizara ya Usalama wa Ndani Karanja Kibicho amepuuzilia mbali madai ya baadhi ya viongozi wanaounga mkono muungano wa Kenya Kwanza kwamba machifu wanatumiwa kununua vitambulisho ili kushawishi upigaji kura katika uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti.

Akizungumza katika mkutano na maafisa wa usimamizi wa serikali ya kitaifa (NGAOs) huko Murang’a, Kibicho alitaja madai hayo kuwa yasiyo na msingi huku akisema serikali haina nia ya kuvuruga uchaguzi.

Alisema kukutana na machifu na wasimamizi wengine ni masuala ya kawaida ya usalama ambayo yako chini ya mamlaka yake.

“Mojawapo ya matokeo ya mkutano wetu na timu ya NGAOs huko Murang’a ni kuharakisha kufungwa kwa kesi za kinidhamu za machifu wasaidizi walioachishwa kazi ili kuhakikisha huduma zimeanza tena katika maeneo madogo yaliyoathiriwa. Hili litafanywa kwa kushauriana na Naibu Makamishna wa Kaunti,” Alisema.

Kibicho alisema lengo la mikutano hiyo ni kuwaelimisha wasimamizi juu ya usalama na na majukumu yao katika kufanya uchaguzi wa kuaminika.

Aliwaambia viongozi washirika wa Kenya Kwanza kuzingatia matamshi yao haswa wakati  wa kampeni zao,yeye  kama kiongozi hana lolote dhidi yao hata ingawa anawarai Wakenya kutochagua viongozi wenye tabia ya kutiliwa shaka.

Pia alitetea kamati ya mpito iliyoundwa hivi majuzi akisema rais ameagizwa na sheria kuunda kamati ya dhana ya kusimamia mpito.