(Video) "Mtafute pa kutorokea jamaa wa kofi akishinda, ana hasira" Sifuna awashauri Wakenya

Sifuna alisema haya baada ya Ruto kumfokea mfuasi wake.

Muhtasari

• Sifuna alisema haya baada ya Ruto kuonekana kwenye video akimfokea kijana mmoja kwenye kampeni zake.

Mkanda wa video wa naibu rais akimtetesha kijana mmoja katika mja ya hafla za kampeni yake imezua mjadala mkali mitandaoni huku baadhi ya viongozi kutoka kwa mrengo wa Azimio-One Kenya waliishabikia kwa kusema kwamba madai yao kuhusu Ruto kujawa na hasira yamedhibitishwa.

Video hiyo  inamuonesha Ruto akiwa amezungukwa na umati wa wafuasi wa Kenya Kwanza katika kaunti ya Vihiga ambapo kijana mmoja miongoni mwa umati alijaribu kumjibu baada ya umati huo kuzua bughudha kutokana na mwanasiasa mmoja ambaye hawakuwa wanamtaka.

Ruto alimjia juu kijana huyo miongoni mwa umati huku akimtupia kidole cha lawama na kumtolea onyo kali kwamba hafai kumjibu.

“Wewe kijana wacha kunijibu, unanijibu kama nani. Kama umeleta kisirani kwa huu mkutano utoke. Huwezi kuja hapa na kuharibu mkutano,” Ruto alionekana akisema huku akikemea tabia ya kijana huyo.

Matamshi haya ya naibu rais yamekuwa gumzo mitandaoni ambapo baadhi ya viongozi wamemshambulia vikali kwa kile walisema ameelekeza hasira zake kwa wananchi wasiokuwa na hatia.

Katibu mkuu wa chama cha ODM Edwin Sifuna amekuwa kiongozi wa hivi punde kumkashfu Ruto na kusema kwamba yeye tayari alishaambia watu watafute mahali pa kujificha endapo Ruto atachaguliwa kama rais.

“Mimi niliwaambia mtatafuta mahali ya kutorokea huyu jamaa ya kofi akipata kiti mkafikiri ni mchezo! Hii hasira yote zile makofi mtakula,” aliandika Edwin Sifuna.

Sifuna ambaye analenga kuwa seneta wa kaunti ya Nairobi kupitia tikiti ya chama cha ODM alimalizia kwa kusema kwamba uzuri anajua hizo hasira za naibu rais William Ruto hazitafanikiwa kwa sababu Raila Odinga anaelekea kushinda uchaguzi huo.

“Bahati nzuri Baba atashinda kwa kura nyingi. Tuko salama. Kenya iko salama,” Sifuna aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.