Malala kuwania ugavana Kakamega baada ya kuponea shoka la mahakama

Wapinzani wa Malala walikuwa wanashinikiza seneta huyo kufungiwa nje ya kinyang'anyiro cha ugavana.

Muhtasari

• Malaal sasa atamenyana nac Ferdinand Barasa, Cyrusc Jirongo, Samwel Omikoka miongoni mwa wengine.

Seneta Cleopas Malala akihutubia wakazi wa Kakamega
Seneta Cleopas Malala akihutubia wakazi wa Kakamega
Image: HILTON OTENYO

Afueni kwa seneta wa kaunti ya Kakamega Cleophas Malala pamoja na wafuasi wake baada ya mahakama ya Kakamega kutupilia mbali kesi mbili tofauti zilizokuwa zimewasilishwa na wakaazi wawili wa Kakamega wakidai kwamba shahada ya masomo ya seneta huyo sio halali.

Akitoa uamuzi huo jaji wa mahakama ya Kakamega  Paul Otieno amesema walalamishi hawakuwa na ushahidi wa kutosha kudhihirisha kuwa stakabadhi za Malala ni ghushi.

Wakaazi hao wawili Fred Muka na Frankline Shilingi waliwasilisha kesi hizo wakiitaka mahakama isimruhusu Malala kuwania  ugavana wakidai kwamba kuna utata kuhusu vyeti vyake vya masomo.

Jaji Otieno pia alisema chuo cha USIU kilitoa ushahidi mbele ya mahakama hiyo kwamba seneta Malala alisoma na kuhitimu na shahada ya Mawasiliano na Utandawazi kutoka chuo hicho kilichopo viungani mwa mji wa Nairobi.

Sasa seneta huyo aliyechaguliwa kwa tikiti ya chama cha ANC ako huru kuendelea na azma yake ya kuwa mrithi wa gavana Oparanya kupitia tikiti ya chama cha UDA.