"Siasa na masomo" Mbunge wa Kandara Alice Wahome avalia sare shuleni

Alice Wahome anawania kutetea kiti chake katika eneo bunge la kandara kupitia chama cha UDA

Muhtasari

• Wiki chache zilizopita mbunge Oscar Sudi pia alionekana katika sare za shule

Mbunge wa kandara Alice Wahome
Mbunge wa kandara Alice Wahome
Image: Facebook

Mbunge wa Kandara mheshimiwa Alice Wahome ameingia katika chama cha wabunge na waheshimiwa walioonekana kwenye sare za shule katika kipindi hiki cha kampeni za kujipigia debe kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Hii ni baada ya Wahome kutia nakshi kwenye sare maridadi ya shule mpya kabisa kwenye eneo bunge hilo, shule ya upili ya Waitua ambayo alikuwa akiifungua kuanza kuhudumia watoto kimasomo rasmi.

Katika rundo la picha alizozipakia kwenye ukurasa wake wa Facebook, Wahome alionekana akiwa miongoni mwa wanafunzi huku kweney video moja akionekana kukata utepe wa kuashiria kufunguliwa rasmi kwa mradi huo uliofadhiliwa na fedha za CDF ya eneo bunge la Kandara chini ya uongozi wake.

“Mwanafunzi nambari moja kwenye shule hii. Ikumbukwe shule ya upili ya Waitua ni miongoni mwa miradi tuliyoianzisha kutoka msingi mpaka kumalizika katika eneo bunge hili la Kandara. Masomo. Masomo. Masomo. Tumetimiza,” Mheshimiwac Wahome aliandika.

Huyu si mheshimiwa wa kuanza kuonekana akizundua miradi ya masomo kwenye shule huku akiwa katika sare za shule kwani wiki mbili zilizopita mbunge wa kapseret Oscar Sudi pia alionekana akiwa ndani ya sare ya shule moja katika eneo bunge lake wakati wa hafla.

Wabunge hawa wote wanaegemea mrengo wa naibu rais William Ruto na wote wanalenga kutetea nyadhifa zao kupitia chama cha UDA katika uchaguzi mkuu ujao wa Agosti 9.