Ruto aagizwa kuomba msamaha kwa kumuita Wamalwa mwanamke

Savula alisema kuwa Ruto lazima aheshimu jamii ya Waluhya.

Muhtasari

•Ruto alipatiwa siku saba za kuomba msamaha la sivyo akabiliane na maandamano makubwa kwa kuwadhalilisha Waluhya.

•Naibu rais alisema kuwa mila za jamii yake ya Kalenjin haziruhusu mwanamume kumpiga mwanamke kofi.

DP RUTO
Image: EZEKIEL AMING'A

Naibu rais William Ruto ameagizwa kuomba msamaha kwa jamii ya Waluhya kwa kumtaja waziri wa ulinzi Eugene Wamalwa kuwa mwanamke.

Mbunge wa Lugari Ayub Savula Jumapili alimpa Ruto siku saba za kuomba msamaha la sivyo akabiliane na maandamano makubwa kwa kuwadhalilisha Waluhya.

“Nataka kuzungumza na Ruto kwa heshima. Sisi kama Waluhya tunataka heshima. Iwapo atashindwa kuomba msamaha ndani ya siku saba, nitaongoza maandamano ya amani dhidi yake kote Magharibi,” alisema.

Alisema kuwa ni bahati mbaya kwa mtu anayetaka kuongoza nchi kukosa heshima kwa jamii nzima, akiongeza kuwa Ruto amejawa na hasira na hafai kuwa rais.

“Tutatumia pesa zote tulizo nazo kuhakikisha kuwa Ruto si rais,” alisema.

Alikuwa akihutubia mkutano wa kampeni katika soko la Mbururu eneo bunge la Likuyani siku ya Jumapili.

Savula ndiye naibu kiongozi wa chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) na mgombea mwenza wa mgombeaji ugavana wa Kakamega ODM Fernandes Barasa.

akihutubia mkutano wa kampeni katika soko la Mbururu eneo bunge la Likuyani Jumamosi
Mbunge wa Lugari Ayub Savula akihutubia mkutano wa kampeni katika soko la Mbururu eneo bunge la Likuyani Jumamosi
Image: HILTON OTENYO

Akihutubia mikutano ya hadhara magharibi mwa Kenya wiki moja iliyopita, Ruto alisema kuwa mila za jamii yake ya Kalenjin haziruhusu mwanamume kumpiga mwanamke kofi.

Alikuwa akijibu madai ya Wamalwa wakati wa mkutano wa Azimio katika uwanja wa Bukhungu wiki moja nenda kwamba nusura ampige kofi katika ikulu ya mwaka wa 2018.

Haya yalijiri wiki moja baada ya video kuvuja ambapo Naibu Rais alisema nusura ampige kofi rais Uhuru Kenyatta baada ya kuashiria dalili za kukata tamaa na marudio ya uchaguzi wa urais mwezi Oktoba 2017.

Wazee wa ukoo wa Wamalwa wa Baengele kutoka eneo la Trans Nzoia pia wamekashifu matamshi ya Ruto na kudhalilisha jamii.

Savula alisema kuwa Ruto lazima aheshimu jamii ya Waluhya.

(Utafsiri: Samuel Maina)