Mgombea ubunge wa Mathare kwa tiketi ya Jubilee Kelvin Kioko almaarufu Bahati amesisitiza kwamba atakuwa kwenye debe katika uchaguzi wa mwezi ujao licha ya kiongozi wa Azimio-One Kenya, Raila Odinga kumtaka amuachie mpinzani wake wa ODM Antony Tom Oluoch.
Jumapili Raila alipokuwa anajipigia debe katika eneo la Mathare alimuidhinisha Oluoch kuwania ubunge wa eneo hilo na kuahidi kumpa Bahati kazi katika serikali yake ikiwa atachaguliwa kuwa rais mnamo Agosti 9.
"Huyu Bahati ni mtoto yangu. Yeye nitampatia kazi katika serikali. Sawasawa. Kwa hivyo sasa mbunge wa Ruaraka ni bwana TJ Kajwang, halafu mbunge wa Mathare ni bwana Oluoch," Raila alisema.
Bahati ambaye alionekana kutoridhishwa na matamshi ya kinara huyo wa ODM aliruka kutoka juu ya gari ambapo walikuwa wamefanya jukwaa na kugura mkutano.
Baadae alizama kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii na kusisitiza kuwa hatatupilia azma yake ya kuwania ubunge.
"Nimeidhinishwa na IEBC na chama changu cha Jubilee.. Nimebarikiwa na Mungu na watu wa Mathare wameamua mbunge anayefuata ni Bahati Kioko," Bahati aliandika kwenye Twitter.
Aliendelea "Mimi Bahati Kioko nitakuwa kwenye debe mnamo Agosit 9!"
Azma ya msanii huyo mwenye umri wa miaka 29 ya kuingia bungeni imekumbwa na matatizo si haba.
Hapo awali alidaiwa kupokonywa kibali chake cha Jubilee na maafisa wa chama hicho licha ya kukabidhiwa awali.
Baadae Bahati alihusika kwenye vita ya maneno na katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna kuhusu uwaniaji wake wa ubunge wa Mathare..
Hii ilikuwa baada ya Sifuna kudai kuwa chama cha Jubilee kilikuwa kimeafikiana na ODM kuachia mgombeaji wa ODM eneo hilo.
Bahati alipuuzilia mbali madai hayo na kusema hatawahi kughairi azma yake.