Gachagua amshambulia Uhuru katika mdahalo na Karua

Gachagua alidai kuwepo njama ya kumfurusha naibu rais William Ruto ili nafasi yake ichukuliwe na Gideon Moi

Muhtasari

• Karua alisema kwamba yeye atakuwa naibu rais anayeheshimu rais wake na kwamba hata kama pataibuka tofauti kati yake na Raila watashughulikia tofauti zao kwa heshima.

• Gachagua alikaribia kusema kwamba wataikabili vikali kisheria familia moja mashuhuri ambayo kulingana naye imewanyanyasa sana wananchi.

Mgombea mwenza wa Kenya kwanza Rigathi Gachagua na mwenzake wa Azimio Martha Karua wakisalimiana kabla ya kuanza kwa mdahalo siku ya Jumanne 19/07/2022.
Mgombea mwenza wa Kenya kwanza Rigathi Gachagua na mwenzake wa Azimio Martha Karua wakisalimiana kabla ya kuanza kwa mdahalo siku ya Jumanne 19/07/2022.

Mgombea mwenza wa Muungano wa Kenya kwanza Rigathi Gachagua amemshambulia rais Uhuru Kenyatta kwa kutumia vibaya mamlaka kwa manufaa yake ya kibinafsi.

Akizungumza katika mdahalo wa wagombea wenza Jumanne usiku na mgombea mwenza wa muungano wa Azimio-One Kenya Martha Karua, Gachagua alidai kuwa reli ya SGR iliongezwa hadi katika eneo la Naivasha kwa minajili ya kuhudumia kampuni moja iliyo na uhusiano wa karibu na familia ya kwanza nchini.

Gachagua ambaye pia ni mbunge wa Mathira alidai kuwa waziri wa fedha aliondolea benki inayomilikiwa na familia moja mashuhuri nchini mzigo wa kulipa serikali takriban shilingi milioni 300.

Gachagua alikaribia kusema kwamba wataikabili vikali kisheria familia moja mashuhuri ambayo kulingana naye imewanyanyasa sana wananchi.

“Kuna kampuni moja ya maziwa ambayo ina ukiritimba wa kuuza maziwa na inanyanyasa sana wafugaji wa ngómbe wa maziwa, kwamfano wananunua lita moja ya maziwa kwa shilingi 42 kwa mkulima na kisha lita hiyo moja ya maziwa inauzwa shilingi 120 katika maduka ya supermarket,” Gachagua alisema.

Gachagua pia alidai kuwa kulikuwa na njama ya kumfurusha naibu rais William Ruto kutoka kwa serikali ili nafasi yake ichukuliwe na Gideon Moi lakini Ruto aliwashinda maarifa.

Kwa upande wake mgombea mwenza wa Azimio Martha Karua alisema kwamba ikiwa  yeye na Raila Odinga watapata nafasi ya kuongoza taifa watahakikisha kwamba wanaziba mianya yote ya ufisadi ili kuboresha uchumi.

Karua alikosoa mgombea urais wa Kenya Kwanza William Ruto kwa kuendelea kuvuruga serikali akiwa ndani huku akisema kwamba ikiwa Ruto hajaridhika na serikali basi angejiuzulu ili kuacha kunufaika na mshahara na marurupu ya kuwa naibu rais na ilhali anapinga serikali hiyo.

Karua alisema kwamba yeye atakuwa naibu rais anayeheshimu rais wake na kwamba hata kama pataibuka tofauti kati yake na Raila watashughulikia tofauti zao kwa heshima.

Anasema hataruhusu majibizano mbele ya umma kati yake na kinara wake.

Karua alidai kuwa viongozi wa Keinya Kwanza wanadoa la ufisadi na hawawezi kuaminika kuongoza taifa.

Karua aliapa kuhakikisiha kuwa katiba inazingatiwa kikamilifu ili kuhakikisiha kuwa kila mtu anapata haki chini ya utawala wao.

"Nitakuwa naibu wa rais ambaye anaheshimu Katiba, watu wa Kenya, wa mkuu wangu na mtu ambaye atatii sheria, na kufanya kila linalowezekana kumuunga mkono nahodha wangu kufanikisha nchi hii," alisema.

Karua alisema atamsaidia kinara wake, Raila Odinga kutii sheria, na kuongeza kuwa kiapo chao kinaelekeza kwamba maslahi ya umma ni muhimu katika kila jambo ambalo serikali hufanya.

Kiongozi huyo wa Narc Kenya alisema atahudumu kwa uaminifu, akidokeza kwamba rekodi yake ya utendaji inaonyesha kuwa amefanya hivyo siku za nyuma.

"Kwamba nimekuwa mtumishi wa umma ambaye anafanya kazi yake kwa njia iliyowekwa na sheria, kwa uaminifu, kwa kujitolea. Nitajitolea kwa asilimia 100 kwa watu wa Kenya," alisema.

Karua na Gachagua walikuwa wakilumbana katika mdahalo ulioandaliwa katika chuo kikuu cha Catholic.