Martha Karua na Rigathi Gachagua wafunguka kuhusu utajiri wao

Wanasiasa hao wawili walifichua kuwa ni mamilionea wakubwa.

Muhtasari

•Karua ambaye ni mgombea mwenza wa Raila Odinga katika uchaguzi wa mwezi ujao alidai kuwa ana thamani ya Ksh 150M.

•Mgombea mwenza wa William Ruto, Rigathi Gachagua alitangaza kuwa utajiri wake ni takriban Ksh milioni 800.

wakizungumza wakati wa mdahalo wa naibu rais katika CUEA mnamo Julai 19, 2022.
Mgombea mwenza wa UDA Rigathi Gachagua na Martha Karua wa Azimio - One Kenya wakizungumza wakati wa mdahalo wa naibu rais katika CUEA mnamo Julai 19, 2022.
Image: RADIO JAMBO

Wagombea wenza Martha Karua wa Azimio-One Kenya na Rigathi Gachagua wa Kenya Kwanza wamefunguka kuhusu utajiri wao.

Wakizungumza Jumanne jioni wakati wa mdahalo wa naibu rais uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Katoliki cha Afrika Mashariki (CUEA), wanasiasa hao wawili walifichua kuwa ni mamilionea wakubwa.

Karua ambaye ni mgombea mwenza wa Raila Odinga katika uchaguzi wa mwezi ujao alidai kuwa ana thamani ya Ksh`150,000, 000.

"Nadhani nina thamani ya takriban  milioni 150. Hii ni kwa sababu utajiri wa milioni 56 ambao niltangaza 2013  umepanda kwa sababu ya mfumuko wa bei,"Karua alisema alipohojiwa kuhusu utajiri wake wa sasa.

Mbunge huyo wa zamani wa Gichugu alibainisha kuwa hajanunua mali mpya katika kipindi cha takriban mwongo mmoja ambacho kimepita.

"Mimi ni mtu ambaye wengi huenda wasimuelewe. Sina tamaa ya ardhi, sina tamaa ya vitu vya dunia. Nina furaha ya kuwa na mahali ambapo naweza kuita nyumbani. Niko na furaha kuwa na nyumba katika ardhi ya baba yangu. Huwa sitafuti mali," Alisema.

Kwa upande wake mgombea mwenza wa William Ruto, Rigathi Gachagua alitangaza kuwa utajiri wake ni takriban Ksh milioni 800.

Gachagua alidai kuwa pesa zake ambazo zinazuiliwa na mahakama kwa madai ya ufisadi ni Ksh200M wala sio Ksh 5B kama inavyodaiwa.

"Milioni 64 nilifanya kazi katika wizara ya ardhi na makazi, 10M nilifanya kazi na Kenya Power, 33M nilifanya kazi katika wizara ya mifugo,milioni zingine 46 nilifanya kazi na shirika lingine linaloitwa Patek , hadi milioni 200," Gachagua alifafanua kuhusu pesa zake zinazoshikiliwa na mahakama tangu 2020

Aliongeza," Niko na 203M katika akaunti inayozuiliwa. Akaunti hiyo ni sehemu ya utajiri wangu. Mimi niko na thamani ya Milioni 800, kuondoa milioni 200 ambazo wanazuilia, na zingine milioni 600.".

Mbunge huyo wa Mathira alipuuzilia mbali madai ya kuhusika kwenye ufisadi na kusisitiza kuwa chanzo kikuu cha utajiri wake mkubwa ni biashara.

"Pesa nilizo nazo zimenakiliwa vizuri. Mimi ni mfanyabiashara anayefanya kazi kwa bidii. Hizi ni pesa nilizopata wakati wa utawala wa Mwai Kibaki wakati uchumi ulipokuwa ukiimarika," Alisema Gachua.

Pia alikana madai ya kujinufaisha kwa kupata zabuni kutoka kaunti ya Nyeri wakati ndugu yake marehemu Nderitu Gachagua alipokuwa gavana.