(Video) Ruto anunua nguo kwa Ksh 20K Gikomba

Ruto alifanya hivo kuonesha utimilivu wa ahadi zake za kuinua biashara za mtaji wa chini.

Muhtasari

• Naibu William Ruto alimkabidhi mfanyibiashara wa Gikomba 20K kama bei ya nguo aliyompatia wakati wa kampeni mapema Jumatatu.

Jumatatu naibu rais na ambaye ni mpeperusha bendera wa urais kutoka muungano wa Kenya Kwanza, William Ruto alikuwa na msururu wa kampeni zake za kuuzia wanqanchi sera zake katika eneo pana la Nairobi.

Katika mkutano mmoja eneo la soko wazi la Gikomba Ruto alipewa koti na mfanyibiashara mmoja na kuilipia kwa shilingi elfu 20 pesa taslimu za benki kuu ya Kenya.

Baada ya kukabidhiwa Koti hiyo, mwaniaji wa ugavana Nairobi kwa tikiti ya chama cha UDA  Johnson Sakaja ambaye alikuwa akizungumza alimsifia kuwa amependeza na Ruto akamtaka mwanamke mfanyibiashara aliyempa ile nguo kuzungumza bei.

“Haya hii si imenitoa vizuri, sasa wacha tuzungumze bei” Ruto alisema kwa utani mwingi.

Mfanyibiashara huyo alimuambia kwamab nguo hiyo kwa sababu yeye ni naibu rais alifaa kutoa shilingi elfu mbili ila Ruto akapinga kidogo kuwa hiyo bei iko juu, kama kawaida ya Wakenya wengi wanapoenda sokoni.

“Hiyo elfu 2 ni nyinhi sana. Nifanyie kwa bei nzuri, bei ya jioni. Huyu mfanyibiashara anataka kuninyoa bila maji. Mimi nimechanuka, hiyo bei ni ghali mno,” Ruto alizua utani katika kuzungumza lugha ya biashara.

Baadae aliingia mfukoni na kutoa bunda la noti ambalo alitaja akimpokeza yule mfanyibiashara akimwambia ‘chukua hii elfu 20 ujipange’

Kitendo hicho kilimpatia sifa nyingi kutoka kwa wafanyibiashara wa mtaji mdogo ambao mwanasiasa huyo amewapa kipaumbele katika manifesto yake akisema kwamba pindi serikali ya Kenya kwanza itakapochukua hatamu kuanzia Agosti 10 basi lengo lake litakuwa ni kuanza kuinua watu wa chini kuelekea juu almaarufu ‘Bottom-Up Economic Model’

Hii si mara ya kwanza Ruto anagusa na kusogeza nyoyo za wafuasi wake kwani wiki jana katika eneo la Samburu alinunua vijiti vinavyotumika kama mswaki na jamii ya eneo hilo kutoka kwa kijana mmoja kwa bei ghali ya shilingi elfu ishirini za Kenya, kama njia moja ya kuonesha kutekelezwa kwa ahadi zake za kukuza na kuinua biashara za chini zenye mtaji wa kuanzia.