Jinsi Gachagua alivyoshambulia Karua kwa kugura serikali ya Kibaki

Kujiuzulu kwa Karua kulijiri baada kuundwa kwa serikali ya nusu-mkate

Muhtasari

•Gachagua alisema kiongozi huyo wa Narc-K hakufaa kukubali shinikizo na kugura serikali ya Kibaki wakati alimpohitaji zaidi.

•Karua alisema aliacha  kazi kwa sababu alikuwa na kanuni zake zilizokuwa zinamuongoza na ambazo zilitofautiana na za Kibaki. 

wakati wa mdahalo wa naibu rais uliofanyika CUEA, Nairobi mnamo Julai 19, 2022.
Rigathi Gachagua na Martha Karua wakati wa mdahalo wa naibu rais uliofanyika CUEA, Nairobi mnamo Julai 19, 2022.
Image: RADIO JAMBO

Mdahalo wa naibu rais ambao uliwakutanisha Martha Karua wa Azimio-One Kenya na Rigathi Gachagua wa UDA hatimaye ulifanyika Jumanne jioni katika Chuo Kikuu cha Katoliki cha Afrika Mashariki (CUEA) huko Karen, Nairobi.

Katika mdahalo huo uliong'oa nanga saa mbili usiku na kuendelea kwa takriban masaa mawili, wagombea wenza hao wa farasi wawili wakuu katika kinyang’anyiro cha urais cha mwezi ujao walizungumzia baadhi ya masuala yanayowakumba Wakenya kwa sasa, wakazungumza kuhusu mipango yao kwa Wakenya iwapo watachaguliwa afisini na hata kushambuliana katika masuala mbalimbali yanayowahusu.

Gachagua ambaye ni mgombea mwenza wa naibu rais William Ruto hakumsamehe mpinzani wake  kwa kugura serikali ya hayari Mwai Kibaki wakati wa muhula wake wa pili kama rais wa tatu wa Kenya.

"Dada yangu Martha Karua aligura serikali ya  Mwai Kibaki wakati ambapo alimhitaji zaidi, wakati Kibaki alikuwa kwenye shida, wakati Raila Odinga alikuwa anafanya maisha yake kuwa magumu," Rigathi alisema.

Karua ambaye ni mgombea mwenza wa Raila katika kinyang'anyiro cha mwaka huu alihudumu kama Waziri wa Sheria na Masuala ya Katiba katika serikali ya Kibaki hadi mwaka wa 2009 wakati ambapo alijiuzulu.

Kujiuzulu kwa Karua kulijiri baada ya kuundwa kwa serikali ya nusu-mkate kufuatia  makubaliano ya Kibaki na Raila kufanya kazi pamoja.

Huku akijitetea wakati wa mdahalo wa Jumanne, Karua alisema aliacha  kazi kwa sababu alikuwa na kanuni zake ambazo zilimuongoza. Alisema kanuni zake na aliyekuwa rais wa tatu zilitofautiana ndiposa akaondoka. 

"Nilijiondoa kwenye serikali ya Kibaki kwa njia ya heshima.. Katika kipindi cha miaka sita unusu ambacho nilihudumu, sikuwahi kudhalilisha serikali ambayo nilitumikia wala rais ambaye nilitumikia. Nilisema mikono yangu imefungwa na nikajiuzulu. Kanuni zangu zilitofautiana na za Mwai Kibaki lakini alichosema kwa umma ni kuwa sikushauriwa. Jinsi walivyojifungia (Kibaki na Raila) na kusuluhisha hatujui. Tunachojua ni kuwa waliokea na uamuzi mmoja," Karua alisema kuhusu madai ya kugura serikali ya Kibaki.

Gachagua hata hivyo alikuwa na maoni tofauti na kusema kiongozi huyo wa Narc-K hakufaa kukubali shinikizo na kugura serikali.

Alisema itakuwa ngumu kwa kiongozi ambaye alishindwa kufanya kazi na Kibaki kuweza kufanya kazi na mtu mwingine yeyote.

"Mwai Kibaki alikuwa muungwana wa siasa za Kenya, mtu mzuri, mtu anayeheshimika na ambaye alisikiliza kila mtu. Kiongozi yeyote ambaye hangeweza kufanya kazi na Kibaki  nashuku sana ikiwa anaweza kufanya kazi na mtu yeyote mwingine," Alisema.

Karua alisema Kibaki na Raila walishindwa kushughulikia masuala ya ufisadi na uadilifu wake hautamruhusu kusalia serikalini.

“Lakini kwa tikiti ya Karua na Raila tutapambana na ufisadi. Raila na Kibaki walitofautiana lakini walisuluhisha masuala yao faraghani, hivyo ndivyo watu wanaoheshimu umma hufanya.”