Wajackoyah: Sitashiriki mdahalo wa urais bila William Ruto na Raila Odinga

Wajackoyah ananadi sera za bangi na kuuza nyama ya fisi, mbwa na nyoka Uchina.

Muhtasari

• Wajackoyah alisema kwamba ni sharti wakuwe meza moja wagombea wote wanne wazungumzie wakenya ili wakenya hao wafanye uamuzi wa maana mnamo Agosti 9.

Mgombea urais kutoka chama cha Roots, wakili msomi George Wajackoyah
Mgombea urais kutoka chama cha Roots, wakili msomi George Wajackoyah
Image: The star

Mgombea urais wa chama cha Roots, wakili msomi George Wajackoyah sasa ametishia kususia mdahalo wa urais iwapo hatawekwa kwenye meza moja na wagombea wanaopigiwa upato zaidi, kinara wa Azximio One Kenya Raila Odinga na kinara wa Kenya Kwanza, William Ruto.

Akizungumza katika kituo kimoja cha redio nchini mapema wiki jana, Wajackoyah aliulizwa kama atahudhuria mdahalo huo wa urais na yeye akasema atahudhuria kwa sharti kwamba pawepo Raila Odinga na Willima Ruto kwenye meza moja ya mdahalo huo.

“Sitohudhuria mdahalo wa urais isipokuwa kama Raila Odinga, William Ruto, David Mwaure na mimi tutakuwa katika meza moja kuzungumza mbele ya Wakenya, ili Wakenya hao ambao ndio wapiga kura kufanya maamuzi yenye busara,” wakili msomi George Wajackoyah alisema.

Ikumbukwe waandaji wa midahalo hiyo wamekuwa wakiwabagua wagomba wa nyadhifa mbali mbali katika vitengo tofauti huku mdahalo wa kwanza ukiwa wa wale wagombea wanaodhaniwa kuwa na ufuasi mchache na mdahalo wa pii wa kumaliza siku ukiwa ule wa wagombea wenye ufuasi mkubwa.

Katika mdahalo wa ugavana Nairobi, wagombea wenye nafasi finyu walianza huku wagombea wakuu ambao ni Johnson Sakaja wa UDA na Polycarp Igathe wa Jubilee wakimenyana katika mdahalo wa mkumbo wa pili.

Juzi katika mdahalo wa wagombea wenza, Justina Wamae ambaye ni mgombea mwenza wa Wajackoyah na Ruth Wamae ambae ni mgombea mwenza wa David Mwaure walifungua jukwaa na baadae usiku wagombea wenza wakuu, Martha Karua wa Raila na Rigathi Gachagua wa Ruto wakamenyana katika kipindi cha lala salama.

Ikumbukwe tayari ratiba ya jinsi mdahalo wa wagombea urais utakavyofanyika ishatolewa huku Wajackoyah na Mwaure wakiwekwa katika kitengo tofauti na Odinga na Ruto, kitu ambacho wakili huyo msomi anayepigia bangi debe amepinga vikali na hata kutishia kususia.

Awali Ruto alikuwa ametishia kususia mdahalo huo kwa kile alitaja kwamba na upendeleo wa vyombo vya habari kwa mshindani wake mkuu Raila Odinga lakini Alhamisi kiongozi huyo wa UDA alidhibitisha kuhudhuria ila akawataka waandaaji wa mdahalo huo kuweka wazi muda utakaopewa kwa kila suala.