Babu Owino: Niko tayari kuwakilisha Raila kwenye mdahalo wa urais dhidi ya Ruto

Owino alisema ako tayari bora Ruto asiseme uongo na kutaja toroli mbele ya msomi.

Muhtasari

• Ijumaa Junet Mohammed alisema kama mdahalo huo hautazungumzia ufisadi, uadilifu na uongozi basi Raila hatashiriki na badala yake atawakilishwa na Babu Owino.

• Babu Owino alikubali na kuapa kumchachafya Ruto mbele ya Wakenya watakaofuatilia mdahalo huo.

Mbunge wa Embakasi East Babu Owino kwenye moja ya kampeni zake
Mbunge wa Embakasi East Babu Owino kwenye moja ya kampeni zake
Image: Facebook//BabuOwino

Mwanasiasa mchanga Babu Owino sasa amekubali maneno ya mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed kwamba watamtuma yeye aende kumwakilisha mpeperusha bendera wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga katika mdahalo wa urais dhidi ya kinara wa Kenya Kwanza, William Ruto.

Ijumaa katika mkutano wa kisiasa kwenye kaunti ya Trans Nzoia, Junet Mohammed alisema kwamba Raila hangehudhuria mdahalo huo kama masharti fulani hayatatimizwa na badala yake akasema Babu Owino ndiye atatumwa kuwakilisha.

“Baba atakuwa kwenye mdahalo ule, na hayo ni maoni yangu si maoni yake, atakuwa kwa mdahalo kama watazungumzia masuala matatu. Kama watazungumzia mambo ya uadilifu, ufisadi na uongozi. Kama kuna mambo mengine basi sisi kama Azimio la Umoja One Kenya tutamtuma mheshimiwa Babu Owino kushiriki kwa niaba ya Baba ili apambane na William Ruto,” Junet alisema kwa kejeli.

Maneno haya yalimfikia babu Owino ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa Azimio la Umoja One Kenya kwenye msafara huo wa kunadi sera za Raila kuelekea uchaguzi wa wiki tatu zijazo, na alionekana kukubali kwa mikono yote miwili huku akisema kwamba atamchabanga William Ruto kwenye mdahalo huo kwa niaba ya Raila iwapo atapewa hiyo nafasi.

“Niko tayari kumkabili Ruto kwenye mdahalo wa urais kwa sharti kwamba hatasema uongo na hatataja neno toroli mbele ya msomi. Nitampeleka kwenye Usahaulifu wa kisiasa ambao ni kuzikwa kwa wasiostahili kwenye mavumbi yao ya utupu,” mbunge huyo wa Embakasi mashariki aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Mdahalo wa wagombea urais unazidi kukumbwa na misukosuko kadha baada ya Ruto jana kutoa sharti kwamba hata kama amekubali kushiriki lakini pia alitaka kufahamu kila suala litapewa muda wa dakika ngapi kuzungumziwa.

Isitoshe, mgombea urais kutoka chama cha Roots, wakili msomi George Wajackoyah naye Ijumaa asubuhi alitishia kususia mdahalo huo kwa kusema kwamab hawezi shiriki kama hawatakuwa na wagombea wengine watatu kwenye meza moja.