(Video) Mwanasiasa avalisha punda nguo za chama na na kuwaweka kwenye kampeni

Gideon Kimaiyo anapania kuwa mbunge wa Keiyo kusini kupitia chama cha UDA.

Muhtasari

• Msimu huu wa kisiasa unazidi kupamba moto huku wanasiasa mbalimbali wakijitupa ulingoni kwa mbinu mbalimbali.

• Siku chache zilizopita Kimani Ichung'wa alionekana akipika chapati kwa banda la mama ntilie.

• Kimaiyo aliweka rekodi mpya baada ya kuwavalisha punda nguo zenye nembo ya chama cha UDA na kuwatumia kwenye msafara wa kampeni zake

Video ya msafara wa kampeni za Gideon Kimaiyo, jamaa anayelenga kuwa mbunge wa Keiyo Kusini imezua vicheko mitandaoni baada ya msafara huo kuonekana ukijumuisha punda ambao walikuwa wamevalishwa nguo zenye nembo ya chama anachotumia kuwania ubunge – UDA.

Punda hao wanaonekana wakitembea kwa mwendo wa aste huku wakionekana wameng’ara kwa nguo za kijani na njano pamoja na kitoroli mgongoni.

Video hiyo imechekesha sana mitandaoni huku kampeni za wanasiasa katika nyadhifa mbalimbali zikiwa zinapamba moto, siku takribani kumi kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Mtangazaji maarufu nchini Kenya, Nick Odhiambo aliyepakia video hiyo alisema kwamba punda hao walikuwa watulivu kusimama wakisubiri fundi cherehani kuchukua vipimo vyao ili kuwashonea nguo hizo.

“Pongezi kubwa kwa fundi cherehani na pongezi kwa punda kwa kuwa mvumilivu wakati vipimo vinachukuliwa,” Nick Odhiambo aliandika kwenye video hiyo aliyoipakia kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Watu walisema kwamba huu ndio ule muda ambao wanasiasa wanajishusha mpaka chini kabisa kwa unyenyekevu ili kunadi sera zao kwa wananchi wa kawaida walio wengi kuwarai wawapigie kura.

Wengine walitaka kumujua fundi cherehani huyo mwenye alipata vipimo kwa njia sahihi na wengine wakitaka kumjua aliyewavalisha punda hao nguo hizo bila kusumbuana kwani punda wanafahamika kuwa Wanyama wenye nongwa sana.

Video hiyo bila shaka ni moja kati ya video nyingi ambazo zimeibuka kipindi hiki cha kampeni zikiwaonyesha baadhi ya wanasiasa wakifanya matukio mbali mbali kama njia moja ya kujisogeza karibu na mioyo ya wapiga kura.

Wiki kadhaa zilizopita mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wa alionekana kwenye video akisaidia mama ntilie wa mgahawa mmoja kupika chapati bandani kwa furaha huku akitqabasamu kwa umati wa wapiga kura waliomzingira kushuhudiwa kioja hicho, kwani si kawaida kuona mtu mashuhuri kama huyo akijinyenyekeza kwa wananchi.

Lakini hii ni kama mbinu moja ya kutafuta kura ambayo imekumbatiwa na wanasiasa wengi wanaounga mkono mrengo wa Kenya Kwanza unaoongozwa na naibu rais William Ruto ambao sera zao zinagusia sana maisha na biashara za watu wa chini huku wakiahidi kwamba pindi watakapochukua uongozi basi wataanza na watu wa chini kupanda juu almaarufu ‘Bottom Up Economic Model’