Ruto alikuwa rafiki yangu lakini sipendi mtu muongo- Uhuru

Rais Uhuru alisema Ruto hawezi kuaminiwa na uongozi wa nchi.

Muhtasari

•Uhuru alisema naibu wake amekuwa akiuza uwongo na kuwataka wananchi kukaa wamoja na kutoyumbishwa na siasa ndogo ndogo.

•Rais alimsuta Ruto kwa kuwadanganya wakazi wa Mombasa na Naivasha kuhusu reli ya SGR na bohari ya kontena ya Inland.

Rais Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta amemshambulia naibu wake William Ruto akimshutumu kwa kile alichokitaja kuwa "kueneza uwongo wa wazi" kwa wananchi.

Huku zikiwa zimesalia siku 11 tu kabla ya uchaguzi wa Agosti, Uhuru alisema Ruto hawezi kuaminiwa na uongozi wa nchi.

Mkuu huyo wa nchi alisema naibu wake amekuwa akiuza uwongo na kuwataka wananchi kukaa wamoja na kutoyumbishwa na siasa ndogo ndogo.

Akizungumzia BBI, Uhuru alisema kuwa Naibu Rais aliwadanganya wananchi ya kwamba mpango huo haukuwa mzuri kwao hivyo basi kuwanyima rasilimali zaidi ambazo zingeweza kuleta usawa.

"Mtu fulani aliwaambia kuwa BBI ilikusudiwa kuniongezea muda wa kukaa, lakini nitarudi nyumbani siku chache zijazo. BBI ilikuwa muhimu kwa watu wetu kwa sababu ingeweza kuleta usawa. Watu wanapigana kwa sababu ya rasilimali," alisema.

Rais pia alimsuta Ruto kwa kuwadanganya wakazi wa Mombasa na Naivasha kuhusu reli ya kiwango cha standard gauge na bohari ya kontena ya Inland.

"Nataka tuambiane ukweli sababu ukweli utakuweka huru. Tumekuwa na rafiki yangu na mimi sichukii mtu yoyote hata kidogo, lakini sipendi mtu wa uongo.

"Wewe unaenda pale Mai Mahiu unawaambia tumejenga reli, alafu unaenda Mombasa unawambia wale walichukua bandari wakapeleka Naivasha. Mimi sipendi hawa watu wa uongo, tunataka watu wa haki."

Rais pia ametoa wito wa kuwepo kwa umoja na amani nchini wakati uchaguzi mkuu unapokaribia.

Rais alishikilia kuwa msimamo wake ni kuunganisha watu wa Kenya kwa ajili ya amani.

Akizungumzia handshake kati yake na Waziri Mkuu huyo wa zamani, rais alisema hatua hiyo ililenga kuleta amani nchini.

"Tuliamua kuja pamoja na Ruto mwaka wa 2013 kutafuta amani na tukapata amani. Kisha nikaenda kumtafuta Raila kwa sababu ya amani, je ilikuwa ni kosa kwangu kufanya hivyo?" Uhuru alihoji.

"Tumekuwa na amani wakati wote, tumekaa pamoja, msidanganywe na siasa ndogo ndogo, hatutaki matatizo, tunataka Kenya ibaki kuwa kitu kimoja."

Kiongozi huyo wa nchi pia aliwataka wananchi kumpigia kura Raila Odinga akisema ameonyesha msimamo wa kweli na anaweza kuaminiwa na uongozi wa nchi katika uchaguzi mkuu ujao.

Pia amewashukuru wakazi wa Nakuru kwa uungwaji mkono mkubwa walioipa serikali ya Jubilee na kumpigia kura katika chaguzi zote mbili za 2013 na 2017.

Kwa upande wake, gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui alimshukuru rais kwa kuifanya Nakuru kuwa kitovu cha kiuchumi.

Kuzinduliwa kwa kituo hicho na ujenzi unaoendelea wa uwanja wa ndege wa Lanet na barabara ya Rironi-Mau Summit utafanya Nakuru kuvutia uwekezaji kwa ajili ya kuboresha kaunti hiyo.

Ukarabati wa reli ya meter gauge ya Nakuru-Malaba ulikuwa ili kuhakikisha usafirishaji wa shehena kutoka Mombasa hadi Malaba.

Reli ya Nakuru-Kisumu ni takriban kilomita 220 na ilikarabatiwa kwa gharama ya 3.8bilioni.