Raila ashikilia uongozi katika umaarufu dhidi ya Ruto- Kura ya maoni

Raila anaongoza kwa 46.7 % huku Ruto akiwa wa pili kwa 44.4%

Muhtasari

•Raila yuko mbele kwa asilimia 46.7, huku William Ruto wa Kenya Kwanza akiwa wa pili kwa asilimia 44.4.

•Muungano wa Azimio-One Kenya unaongoza kwa umaarufu dhidi ya washindani wao wakuu Kenya Kwanza.

Kinara wa ODM Raila Odinga
Image: RAILA ODINGA/TWITTER

Wapiga kura wengi wangemchagua mgombea urais wa Azimio la Umoja- One Kenya Raila Odinga ikiwa uchaguzi ungefanyika leo, kura ya maoni ya Tifa Research imeonyesha.

Katika matokeo ya kura ya maoni yaliyotolewa Ijumaa, Raila yuko mbele kwa asilimia 46.7, huku William Ruto wa Kenya Kwanza akiwa wa pili kwa asilimia 44.4.

Profesa George Wajackoyah wa Roots Party anakuja katika nafasi ya tatu kwa asilimia 1.8.

Mgombea urais wa chama cha Agano Waihiga Mwaure ndiye wa mwisho kwa asilimia 0.1.

Asilimia 5.2 ya wapiga kura bado hawajafanya maamuzi kuhusu chaguo lao la rais katika uchaguzi ujao. Wengine 1.9 walikosa kutoa majibu.

Tifa ilibainisha kuwa umaarufu wa Raila umeongezeka katika maeneo yote tisa isipokuwa eneo la Kati mwa Bonde la Ufa, kutoka kwa utafiti wao wa mwisho.

"Ikilinganishwa na matokeo ya utafiti wa Tifa wa Juni, mgawanyo wa nia iliyoonyeshwa ya kumpigia kura Odinga umebadilika kwa kiasi fulani kote nchini kwa kuwa amepata katika kanda zote tisa mbali na Central Rift (-5%), mafanikio yake makubwa yakiwa Kusini mwa Bonde la Ufa, Nyanza, Magharibi na Mashariki ya Chini. (+15%, 13%, +13 na +12% mtawalia)" Tifa alisema.

Umaarufu wa Ruto tangu utafiti wa mwisho wa Tifa mwezi Juni pia umeongezeka katika kanda sita kati ya tisa, haswa katika uwanja wake wa nyumbani.

"Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, umaarufu wa mgombeaji urais wa DP Ruto umesalia katika hali moja."

Utafiti huo ulisema idadi ya watu ambao hawajaamua imepungua, ambayo ilitokana na mbinu ya ana kwa ana ya kukusanya data.

Kura hiyo ya maoni ilikuwa na ukingo wa makosa wa  +/- 2.16.

Hakuna kura mpya ya maoni inayoweza kuchapishwa chini ya siku tano kabla ya uchaguzi, kulingana na sheria. 

Kwa hivyo siku ya mwisho ya kura yoyote ya maoni kuchapishwa itakuwa tarehe 4 Agosti.

Muungano wa Azimio la umoja pia unaongoza kwa umaarufu dhidi ya washindani wao wakuu wa Kenya Kwanza.

Asilimia 47 ya wapiga kura wanaunga mkono muungano wa Azimio huku asilimia 42 wakiegemea upande wa Kenya Kwanza.

Asilimia 5 hawaungi mkono muungano wowote ilhali asilimia 6 wengine wakiwa hawajafanya maamuzi yao bado.