Maisha yangu yamo hatarini!- Rigathi Gachagua adai

Mgombea mwenza huyo wa Ruto anadai kuwa watu fulani wamekuwa wakifuatilia mienendo yake.

Muhtasari

•Gachagua anadai kuwa watu fulani wamekuwa wakifuatilia mienendo yake  huku akitaja kisa cha Nakuru ambapo alikuwa ameenda kukampeni.

•Mbunge huyo wa Mathira sasa amemtaka Rais kufikiria kustaafu kwa amani kwa kuwa muda wake unakaribia kumalizika.

Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua
Image: EUTYCAS MUCHIRI

Mbunge wa Mathira na mgombea mwenza wa urais wa UDA Rigathi Gachagua sasa anasema maisha yake yamo hatarini.

Gachagua anadai kuwa watu fulani wamekuwa wakifuatilia mienendo yake  huku akitaja kisa cha Nakuru ambapo alikuwa ameenda kupeleka kampeni za Kenya Kwanza.

Mgombea mwenza huyo wa Ruto, hata hivyo, alisema hataogopa na ataendelea kushinikiza azma yao ya urais.

"Sababu ya mimi kusema maisha yangu yako hatarini ni kwamb watu fulani wamekuwa wakinifuata, kisa cha hivi majuzi mjini Nakuru. Lakini siogopi, niko tayari kulipa gharama kubwa," Gachagua alisema akiwa kwenye kampeni. katika kaunti ya Nyeri.

Kulingana na Gachagua, Rais Uhuru alifanya mkutano wa siri ambapo alisema atawapa somo yeye pamoja na wabunge Moses Kuria (Gatundu Kusini) na Ndindi Nyoro (Kiharu) somo.

Mbunge huyo wa Mathira sasa amemtaka Rais kufikiria kustaafu kwa amani kwa kuwa muda wake unakaribia kumalizika.

Gachagua ambaye alikuwa ameandamana na viongozi wa Kenya Kwanza alitoa imani kwamba watashinda uchaguzi wa Agosti 9.

Jumamosi asubuhi mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria  aliibua madai kuwa Rais Uhuru Kenyatta anatishia maisha yake.

Kuria kwenye taarifa ya kupinga Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai alidai kuwa maisha yake yamo hatarini. 

Mbunge huyo mwenye utata alimkosoa IG wa polisi kwa kumpa usalama wa ziada mgombeaji wa ugavana Kiambu wa UDA Kimani Wamatangi katika mikutano yake yote ya kisiasa.

Ni wakati akitoa kauli hiyo alidai Rais alimtishia.

"Ndugu IG Mutyambai, huku bosi wako Uhuru Kenyatta akiwa na shughuli nyingi za kutishia maisha yangu, unawapa polisi waliovalia sare kwenye magari matatu chini ya uongozi wa OCS kwa mshindani wangu Kimani wa Matangi kwa mikutano yake yote," alisema kupitia taarifa aliyopakia Facebook Jumamosi.

"Ilifanyika Jumatano huko Mungere huko Lari na jana Ngegu, Kiambu Mjini. Hata Gavana James Nyoro hapati kiwango hiki cha usalama. Tutendee sote kwa usawa na zaidi sisi ambao maisha yao yako hatarini baada ya vitisho vya Uhuru Kenyatta."

Kuria hata hivyo, hakufichua ni kwa nini alitishiwa na rais.