Uhuru ajibu madai ya kupanga kumuua Ruto na washirika wake

" Si mmenitusi karibu miaka tatu? Kuna mtu ambaye amewaguza?" Uhuru alihoji.

Muhtasari

•Uhuru aliweka wazi kuwa anakusudia kustaafu kwa amani na hana mpango wa kumuua mtu yeyote.

•Rais ameiomba kambi ya Ruto ya Kenya Kwanza kusitisha matusi na kutoa wito kwa kampeni za amani.

Rais Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta amepuuzilia mbali madai ya kupanga njama ya kumwangamiza naibu wake William Ruto pamoja na washirika wake.

Akizungumza Jumapili katika hafla ya uzinduzi rasmi wa barabara kuu ya Nairobi Express Way, Uhuru aliweka wazi kuwa anakusudia kustaafu kwa amani na hana mpango wa kumuua mtu yeyote.

Mkuu wa nchi alibainisha kuwa alikuwa na uwezo wa kufanya hivyo katika siku kipindi cha utawala wake ila hakulitekeleza.

"Hakuna haja ya matusi, hakuna haja ya kuingilia watu. Na nikikujibu kwa sababu umesema mambo ya uwongo, hakuna haja ya kusema eti nataka kukuua. Si mmenitusi karibu miaka tatu? Kuna mtu ambaye amewaguza?" Uhuru alisema.

Alisema kuwa hana muda wala uwezo wa kupanga mauaji kama ilivyodaiwa na mgombea urais wa UDA na wandani wake kadhaa.

Rais pia aliiomba kambi ya Kenya Kwanza kusitisha matusi na kutoa wito kwa kampeni za amani huku ikiwa imesalia siku chache tu uchaguzi kufika.

"Hakuna haja ya matusi jameni. Kila mtu akiwemo mimi mwenyewe ako na Uhuru wa kupigia debe yeyote ambaye anataka. Kwa hivyo, wewe unampigia huyu, mwingine anampigia huyu.Uamuzi utakuwa wa wananchi," Alisema.

Vilevile alitoa wito kwa Wakenya kudumisha amani kabla na hata baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Wiki iliyopita naibu rais, mgombea mwenza wake Rigathi Gachagua na wabunge Ndindi Nyoro na Moses Kuria walimshtumu rais kwa kutishia maisha yao.

Akizungumza mjini Kapsabet Ijumaa, Ruto alimrai bosi wake kudumisha heshima kati yao na kumuomba asidhuru watoto wake.

"Rafiki yangu bwana rais, tafadhali kuwa muungwana. Kuwa na shukrani, sisi ndio tulikusaidia.  Tafadhali.. Wacha kujifanya saa hizi sijui unajifanya nini. Eti sasa wewe unaanza kunitishia mimi! Eti utanifanya nini.. bora usidhuru watoto wangu. Lakini mimi na wewe tuheshimiane tafadhali," DP alisema.

Ruto alimwambia Uhuru kuwa hahitaji uungwaji mkono wake katika kinyang'anyiro kijacho na kumtaka aachane naye.

"Mimi ni Mkristo. Mimi sitakuwa na maneno na wewe. Nitahakikisha kuwa umeenda nyumbani polepole na upumzike uendelee na maisha yako uniachie Kenya hii niiskume mbele," Alisema.

"Wachana na William Ruto. Nilikuunga mkono wakati ulinihitaji. Kama hutaki kuniunga mkono niache! Tafadhali!"

Jumamosi mgombea mwenza wake Rigathi alisema maisha yake yamo hatarini huku akidai kuwa watu fulani wamekuwa wakifuatilia mienendo yake.

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria aliibua madai kama hayo hayo kupitia ukurasa wake wa Facebook.