"Mkituzuia kuingia Nyayo, tutakongamana katikati mwa jiji la Nairobi" - Moses Wetangula

Wetangula alisema Kenya Kwanza ilitumia kiasi cha Ksh 1.5M kulipia kibali cha Nyayo lakini wamenyimwa.

Muhtasari

• "“Tumeshatambua makutano ya barabara ya Moi na Kenyatta kuwa sehemu ya kukongamana" - Moses Wetangula

Seneta wa Bungoma, Moses Wetangula
Seneta wa Bungoma, Moses Wetangula
Image: Facebook//William Ruto

Kinara wa chama cha FORD-K ambaye pia ni seneta wa Bungoma Moses Wetangula amesema kwamba walilipia uga wa Nyayo jijini Nairobi kiasi cha pesa zaidi ya milioni moja kwa minajili ya kuandaa hafla yao ya mwisho ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wiki kesho ila wanasikia kwamba watazuiwa kukongamana katika uga huo.

Wakili huyo ambaye ni mmoja wa vinara wa muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na William Ruto alisema ikitokea kwamba wamezuiwa kuandaa mkutano wao mkubwa wa mwisho katika uwanja wa Nyayo basi hawatakuwa na budi ila kukongamana katikati mwa jiji la Nairobi.

“Tulituma maombi ya kupewa idhini ya uwanja ule na kulipia kima cha shilingi milioni 1.5 kwa ajili ya mkutano wetu wa mwisho siku ya Jumapili. Ghafla kama chafya tunasikia tunaambiwa kwamba uga huo utatumiwa kuandaa maombi ya kitaifa ya amani siku hiyo. Mshatoa kibali Kasarani kwa washindani wetu. Mmefunga Kamkunji kwamba itatumika na watu wengine. Kama ambavyo tumesema siku mbili zilizopita, kama hamtafungua Nyayo kwa Kenya Kwanza kuandaa mkutano, basi tutakongamana katikati mwa jiji la Nairobi,” alisema Seneta Wetangula.

Alizidi kusema kwamba tayari mipango ishawekwa tayari na kwamba wameshakubaliana makutano ya barabara ya Moi na Kenyatta katikati mwa jiji ndio sehemu watakayokongamana na kutatiza shughuli za kawaida jijini.

“Tumeshatambua makutano ya barabara ya Moi na Kenyatta kuwa sehemu ya kukongamana na nyinyi kama serikali mtajukumika kuwalinda wakenya wote na biashara zao katika mitaa ya Nairobi jijini. Tutafanya hivyo kama ambavyo tulifanya juzi kati katika mji wa Eldoret, Kakamega wakati mlitunyima kibali kuingia Bukhungu,” alitishia Wetangula.

Wetangula alisema kwamba mkutano wao jijini utakuwa kama ule wa rais wa 44 wa Marekani Barrack Obama aliowahutumia watu katika jiji la Berlin saa chache kuelekea ushindi wake mwaka 2008.