Mwaniajia wa Jubilee Embakasi East ajiondoa kinyang'anyironi, amuunga mkono Mureithi wa UDA

Maina Waruinge alikuwa anawania ubunge kwa tikiti ya chama cha Jubilee ila jana alijiondoa na kuamua kumuunga mkono Francis Mureithi

Muhtasari

• Wengi wanahisi hili hi ongezeko la tija kwenye upande wa Mureithi wa UDA  katika safari ya kumbwaga Babu Owino wa ODM.

Wanasiasa Waruige, Waititu, Mureithi katika jukwaa moja la kukaribisha Waruige ndani ya UDA
Wanasiasa Waruige, Waititu, Mureithi katika jukwaa moja la kukaribisha Waruige ndani ya UDA
Image: Facebook//WilliamSamoeiRuto

Naibu rais William Ruto ambaye pia ni mpeperusha bendera wa muungano wa Kenya Kwanza kuelekea uchaguzi mkuu wa wiki kesho amethibitisha kwamba mgombea ubunge wa chama cha Jubilee eneo bunge la Embakasi Mashariki, Maina Waruinge ametupilia mbali azma yake ya kuwania ubunge na sasa atamuunga mkono Francis Mureithi wa UDA katika kumenyana na mbunge wa sasa wa ODM Babu Owino kwenye kinyang’anyiro cha wiki kesho.

Ruto alitangaza hayo kupitia ukurasa wake rasmi wa Facebook, muda mchache baada ya kumalizikia kwa hafla ya maombi iliyofanyika katika makazi yake rasmi eneo la Karen ambako alionekana akitokwa na machozi katikati ya maombi hayo yaliyokuwa yakiongozwa na watumishi wa Mungu.

Baadae baada ya kuelekea kwenye muendelezo wa kampeni kujipigia debe katika maeneo mbalimbali jijini Nairobi, aliweka wazi kwa kupakia picha za Waruige akivalishwa kofia yenye nembo ya UDA jukwaani mbele ya kadamnasi. Waruinge sasa ni mshirika wa Mureithi na wala si mshindani tena. 

“Mgombea ubunge wa Embakasi Mashariki wa Jubilee Maina Waruinge ajiondoa kwenye kinyang'anyiro na kujiunga na UDA ili kumuunga mkono Francis Mureithi,” Ruto aliandika kwenye Facebook.

Ikumbukwe tafiti za hivi karibuni zimekuwa zikiwaonesha washindani Babu Owino na Francis Mureithi wakiwa na ushindani mkali huku umaarufu wao ukiwa umeachana kwa asilimia chache mno.

Ushindani huu ulianza mwaka 2017 katika uchaguzi mkuu ambapo Mureithi kipindi hicho alikuwa anawania kwa tikiti ya chama cha Jubilee na alishindwa kwa kura chache na Babu Owino ambaye ni mbunge wa sasa. Mureithi alielekea mahakamani na kesi inachukua muda mrefu huku ikifika mpaka mahakama ya upeo wa juu ila mwisho wa siku ushindi wa Owino ukahalalishwa.

Hili lilionekana kumshtua mbunge Babu Owino ambaye alifika kwenye ukurasa huo wa Ruto wa Facebook na kusema kwamba hata waungane vipi bado hawawezi kumng’oa.

“Mimi hamniwezi hata Wewe mwenyewe usimame Embakasi East Republic,” Babu Owino alionekana kuachia vitisho baridi.