Raila aliniokoa dhidi ya Ruto na wandani wake - Uhuru

Uhuru alisema alikuwa amebanwa na Naibu wake William Ruto na washirika wake

Muhtasari

• "Uzee sio ugonjwa, lengo ni mtu mwenye masilahi ya nchi. moyo, mtu mtulivu, na ambaye lengo lake ni kazi yake," alisema.

Rais Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta amesema mgombea urais wa Azimio - One Kenya Raila Odinga alimuokoa wakati adui zake walipokuwa wanamfuata. 

Akizungumza na wakazi wa Bungoma siku ya Jumanne, Uhuru alisema alibanwa na Naibu wake William Ruto na washirika wake ambao alidai hawataki kufanya kazi. 

"Si mmeona vile mimi nimekimbizwa na mtu ambaye hana haja na kazi, nimekimbizwa mpaka nimetoa jasho, mpaka Baba amekuja kuniokoa, mnaelewa vile nasema."

 “Nyinyi nyote mmeona jinsi nilivyokuwa nikibebwa na mtu ambaye hataki kufanya kazi, hata jasho lilinitoka, Raila ndiye alikuja kuniokoa upande wa pili, mnaelewa ninachosema,” alisema.

Pia aliwatahadharisha kutowapigia kura wezi la sivyo watajuta. Uhuru, huku akipigia debe uungwaji mkono kwa Raila, alitoa wito kwa kura sita, akisema hiyo itakuwa na ufanisi katika kuendesha serikali.

"Nawaomba kwa heshima, kama mtamuunga Baba (Raila) mkono, mpatieni jeshi lake ili aanze.

Uhuru aliendelea kusema kuwa wananchi hawapaswi kumhukumu mtu kulingana na umri wake linapokuja suala la uongozi wa nchi. Aliwatadharisha wananchi dhidi ya kumchagua mtu mwenye tamaa, aliye na maneno matamu tu yasiyo na vitendo.

 "Mimi bado ni rais, ni mzee na nimeongoza, kulikuwa na vijana ambao wangeweza kufanya kazi hiyo, walikuwa wapi? Uzee sio ugonjwa, lengo ni mtu mwenye masilahi ya nchi. moyo, mtu mtulivu, na ambaye lengo lake ni kazi yake," alisema.