Ukristo sio machozi,Ukristo ni tabia-Karua amsuta Ruto

Aliwaomba wale waliotilia shaka imani yake wangojee siku ya hukumu.

Muhtasari
  • Karua alibainisha kuwa amekuwa katika siasa kwa muda mrefu na kuongeza kuwa yeye ni Mkristo mwenye bidii

Mgombea mwenza wa urais wa Azimio Martha Karua amemsuta Naibu Rais William Ruto baada ya kuangua kilio katika ibada ya maombi huko Karen, Nairobi, Jumanne.

Karua, alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa kampeni katika uwanja wa Bukhungu siku ya Jumatano, alisema watu wanapaswa kuacha kujifanya Wakristo.

Karua alidokeza kuwa uthibitisho wa Ukristo sio jina au kuhudhuria ibada za kanisa.

"Ukiristo sio machozi. Ukiristo ni tabia,unapaswa kujua kwamba esu hana naibu nchini. Wewe wacha kujifanya deputy wa Jesus Christ."

Kiongozi huyo wa NARC Kenya alisema ikiwa mtu anadai kuwa Mkristo, anapaswa kufuata kile ambacho Biblia inafundisha.

"Niwaeleze kwa Bible, Yesu alisema sio kila mtu anaitana Yesu, Yesu ataingia kwa ufalme wa mbinguni."

Karua alibainisha kuwa amekuwa katika siasa kwa muda mrefu na kuongeza kuwa yeye ni Mkristo mwenye bidii.

Aliwaomba wale waliotilia shaka imani yake wangojee siku ya hukumu.

"Penda watu. Wacha kiburi. Wacha vitisho. Kuwa mtu wa kunyenyekea vile kristo alikua ananyenyekea."

Wakati huo huo, alimtetea bosi wake Raila Odinga akisema yeye ni Mwanglikana, Mkristo.

"Tuacheni tuzingatie siasa zenu. Wacheni Wakenya. Acheni kulisonga taifa letu na ufisadi. Wacha watu wangu waondoke!" Karua alisema.

Katika video iliyosambaa siku ya Jumanne, Ruto anaonekana akiingia katika hali ya maombi huku machozi yakitiririka mashavuni mwake.

Wakati fulani, DP anaonekana akiweka mikono yake usoni huku akipepesa macho na macho yaliyojaa maji, jambo ambalo linaweza kuashiria alikuwa akipigana na machozi.