logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Jinsi mauji ya Chris Msando yanavyoendelea kuandama Uchaguzi wa 2022

"Wafanyikazi wetu katika tume, hasa [wale] walio katika kitengo cha teknolojia ICT wana hofu... Ninataka tu kuwasihi wale wanowatisha kuwacha kufanya hivyo'' ,Wafula Chebukati aliwaambia wanahabari.

image
na Radio Jambo

Yanayojiri05 August 2022 - 04:15

Muhtasari


• Kwa urafiki na utulivu, Msando alikuwa akitangaza katika vituo vya runinga vya hapa nchini, akionyesha hatua alizochukua kuhakikisha uchaguzi hauibiwi.

• "Wapiga kura waliokufa hawatafufuka chini ya usimamizi wangu ," alisema katika mahojiano.

Chris Msando, mkuu wa teknolojia katika tume ya uchaguzi ya Kenya, aliuawa miaka mitano iliyopita

Uchaguzi uliotiliwa shaka Pamoja na mauaji ya kutisha ya afisa mkuu aliyesimamia teknolojia ya upigaji kura mwaka wa 2017 bado yanaikera Kenya, kabla ya uchaguzi wiki ijayo.

Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na Mipaka amekuwa akijaribu mara kwa mara kuwahakikishia wananchi wenye wasiwasi kwamba tume yake inaweza kusimamia uchaguzi wa haki, lakini pia amekuwa akionya kuhusu kampeni iliyoratibiwa hasa kwenye mitandao ya kijamii kuwakashifu na kuwatisha wafanyakazi wake.

"Wafanyikazi wetu katika tume, hasa [wale] walio katika kitengo cha teknolojia ICT wana hofu... Ninataka tu kuwasihi wale wanowatisha kuwacha kufanya hivyo'' ,Wafula Chebukati aliwaambia wanahabari.

Ana sababu za msingi za kuwa na wasiwasi: miaka mitano iliyopita mkuu wake wa teknolojia wakati huo, Chris Msando, alitekwa nyara na kuuawa kikatili, pamoja na rafiki yake Carol Ngumbu mwenye umri wa miaka 21.

Miili yao ilipatikana vichakani viungani mwa mji mkuu, Nairobi - na hakuna mtu aliyekamatwa au kushtakiwa kwa mauaji hayo ambayo yamegubikwa na siri.

"Hakika tukiwa na huduma ya polisi yenye utaalamu wa juu na serikali yenye weledi na ufanisi nadhani tungefaa kujua ukweli kuhusu tukio hili ... Taifa halijui ni nani aliyechukua maisha ya afisa wa uchaguzi ambaye alikuwa akishughulikia sehemu nyeti sana ya uchaguzi," alisema Mkurugenzi mkuu wa shirika la haki za kibinadamu la Amnesty International Kenya akizungumza na kituo kimoja cha runinga nchini humo.

Kwa urafiki na utulivu, Msando alikuwa akitangaza katika vituo vya runinga vya hapa nchini, akionyesha hatua alizochukua kuhakikisha uchaguzi hauibiwi.

"Wapiga kura waliokufa hawatafufuka chini ya usimamizi wangu ," alisema katika mahojiano.

Alikuwa ameweka imani yake katika data za kibayometriki ili kuthibitisha wapiga kura kwa kutumia alama za vidole na mfumo wa kielektroniki kusambaza matokeo.

Utumiaji wa teknolojia kama hiyo ulikubaliwa kufuatia kudorora kwa uchaguzi wa 2007 wakati shutuma za ujazo wa kura zilizusha ghasia za wiki kadhaa ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 600,000 kutoroka makazi yao. Wakati huo mwenyekiti wa tume ya uchaguzi wakati huo alikiri hakuwa na uhakika ni nani aliyeshinda.

Uchaguzi huu pia unaonekana kuwa kinyang'anyiro kikali cha urais - kati ya vinara Raila Odinga, kiongozi wa upinzani wa muda mrefu ambaye anawania kwa mara yake ya tano, na Naibu Rais William Ruto.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved