Ruto apokea wagombea wa ugavana na uwakilishi wa kike Embu kuingia UDA kutoka Jubilee

Wikendi iliyopita, Ruto alimkaribisha Maina Waruige kutoka Jubilee kuja UDA katika eneo bunge la Embakasi East.

Muhtasari

• Ruto aliwakaribisha wawili hao na kusema kwamba kweli wimbi la Hustler Nation ni la kweli.

Ruto akiwapokea Susan Nyaga na Emilio Kathure kutoka Jubilee kujiunga na UDA
Ruto akiwapokea Susan Nyaga na Emilio Kathure kutoka Jubilee kujiunga na UDA
Image: Facebook//WilliamSamoeiRuto

Mpeperusha bendera wa urais kutoka muungano wa Kenya Kwanza kupitia chama cha UDA William Ruto ametangaza kuwapokea wanasiasa mbalimbali waliogura muungano pinzani wa Azimio la Umoja One Kenya na kujiunga na kambi yake ya Kenya Kwanza.

Akiwa katika kaunti ya Embu kuzidi kurindima ngoma za sera zake siku chache tu kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, Ruto alitangaza kuwapokea mgombea ugavana Embu kwa tikiti ya Jubilee Emilio Kathuri aliyetupilia mbali azma yake ya kuwa gavana na sasa ameanza rasmi kumuunga mkono mgombea ugavana kutoka chama cha UDA, Cecily Mbarire.

Ruto pia alitangaza kumpokea Susan Nyaga aliyekuwa aliyekuwa akigombea uwakilishe wa wanawake katika kaunti ya Embu kwa tikiti ya chama cha Jubilee na ambaye sasa ameweka pembeni tikiti yake na kujiunga na Kenya Kwanza kumuunga mkono Pamela Njoki ambaye alikuwa mshindani wake awali.

"Wimbi la Hustler Nation ni la kweli! Mgombea ugavana wa Embu Jubilee Emilio Kathuri amejiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho na sasa anamuunga mkono Cecily Mbarire wa UDA. Susan Nyaga (Jubilee) pia ameachana na azma yake ya kuwania kiti cha Mwakilishi wa Wanawake na kumpendelea Pamela Njoki. Karibu," Ruto alitangaza kupitia Facebook yake.

Zikiwa zimesalia siku tatu tu kuelekea uchaguzi mkuu, haijulikani ni kwa nini wanasiasa mbali mbali wanaachia kampeni zao za muda mrefu njiani kabla ya kufika kwenye utepe na badala yake wakijiunga na washindani wao.

Katika Sakata hili, chama cha Jubilee ndicho kinaonekana kuathirika pakubwa ambapo wikendi iliyopita pia aliyekuwa akigombea ubunge Embakasi Mahsariki kwa tikiti ya chama cha Jubilee, Maina Waruinge alitangaza kuacha azma hiyo na kuungana na Francis Mureithi wa UDA.

Katika kaunti ya Kisii, mgombea mwenza wa Manson Oyongo Nyamweya anayelenga kuwa gavana wa kaunti hiyo pia aligura na kumuacha Nyamweya katika njia panda.

Juzi kati, mgombea mwenza wa Sam Ongeri kwenye kaunti hiyo pia alitangaza kugura kambi ya Ongeri ya DAP-K na kujiunga na mpinzani wake mkubwa kutoka UDA, Ezekiel Machogu Ombaki.